Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikabidhi Tuzo maalumu Meneja Mkazi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Paul Atallah (wa pili kushoto), kwa niaba ya kampuni hiyo na Qatar Foundation kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kusaidia watu wenye uhitaji.


Na Dotto Mwaibale, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa Tuzo maalum kwa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar na Qatar Foundation kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kusaidia watu wenye uhitaji.

Dkt. Mwinyi alitoa tuzo hizo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu yaliyofanyika Desemba 4, 2025 kwenye Ukumbi wa Dr. Shein – Tunguu, Chuo Kikuu cha SUZA, Mkoa wa Kusini Unguja tukio lililohudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo, mashirika ya kijamii, na wananchi kutoka sehemu mbalimbali za Zanzibar.

Akihutubia katika maadhimisho hayo Rais Mwinyi aliwataka wadau kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwawezesha watu wenye ulemavu na alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli ni yale yanayowahusisha watu wote bila kuacha kundi lolote nyuma.

Aidha, Dkt. Mwinyi alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wadau na wahisani kwa kujitolea kwao kuchangia maendeleo ya jamii zenye watu wenye ulemavu na kueleza kuwa Serikali itayafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa kamili za kutimiza malengo yao.

Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Paul Atallah, alilishukuru Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar kwa kutambua mchango wa Emirates Leisure Retail na kueleza kwamba kampuni hiyo itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Serikali na jamii katika kuleta maendeleo chanya kwa watu wenye ulemavu.

Utambuzi wa Wadau Maalumu

Katibu Mtendaji wa Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe, akizungumza kwenye maadhimisho hayo alitoa shukrani kwa wadau wote wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia watu wenye ulemavu.

Aidha, kwa nafasi ya kipekee alimshukuru Afisa Utawala Msaidizi wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Ramadhan Hussein Layya (Maarufu Msokolo),kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu, hususan katika kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi kupitia misaada, ushiriki, na michango inayobadilisha maisha ya wanufaika.

Kaulimbiu ya Maadhimisho:

"Uwezeshaji na Ushirikishwaji wa Watu Wenye Ulemavu kwa Maendeleo Jumuishi."

Misaada Iliyotolewa katika maadhimisho hayo kwa ajili ya makundi mbalimbali ya wahitaji ni

Vyerehani kwa ajili ya kujiajiri, kofia maalumu (round hats) kwa ulinzi wa ngozi, miwani ya kinga na vifaa vya kurekebisha uoni, baiskeli za mwendo kwa watu wenye ulemavu wa viungo, fedha za mikopo kwa kuanzisha au kuendeleza biashara.

Vifaa vingine vilivyotolewa ni vya kuongeza uwezo wa kujitegemea mashine za kusaga nafaka.

Misaada hiyo imeleta furaha, matumaini, na thamani kubwa kwa wanufaika na familia zao, ambayo inakwenda kuwasaidia kutimiza ndoto zao na kuimarisha ustawi wa familia zenye watu wenye uhitaji maalumu.

Kauli ya Emirates Leisure Retail Zanzibar na Qatar Foundation:

Uongozi wa kampuni hizo umeeleza dhamira zao za kuendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha watu wenye ulemavu Zanzibar wanapata fursa sawa za ustawi na maendeleo, na kuendelea kuwekeza katika miradi ya kijamii inayobadilisha maisha ya watu wenye uhitaji maalumu.
Viongozi wa Kampuni hizo na wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...