Farida Mangube Morogoro.

MKUU wa Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, Japhari Kubecha, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani humo kwa kazi nzuri wanayofanya katika ukusanyaji wa mapato ya serikali, akisisitiza kuwa juhudi hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza ofisini kwake baada ya kutembelewa na Meneja wa TRA Wilaya ya Gairo, Ditram Wila, pamoja na Afisa Mwandamizi Elimu na Mawasiliano wa TRA Mkoa wa Morogoro, Immaculate Chaggu, waliofika kumpatia zawadi ya Ushirikiano wa mwaka 2025 kutokana na mshikamano aliouonyesha kwa mamlaka hiyo, DC Kubecha alisema TRA imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wafanyabiashara wanatimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati.

Aidha, alieleza kuwa ushirikiano mzuri kati ya TRA, wafanyabiashara na viongozi wa serikali ni msingi muhimu wa mafanikio katika ukusanyaji wa mapato. Alibainisha kuwa kwa kushirikiana kwa karibu, serikali inanufaika kwa kupata mapato yanayohitajika huku wafanyabiashara wakiendesha shughuli zao katika mazingira ya haki, uwazi na yenye kuaminika.

Wafanyabiashara wa Wilaya ya Gairo nao wamepongeza juhudi za TRA, wakisema kuwa elimu ya kodi inayotolewa mara kwa mara pamoja na utaratibu mzuri wa ukusanyaji wa mapato, umesaidia kupunguza changamoto za kibiashara na kuongeza uaminifu kati yao na mamlaka hiyo.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Wilaya ya Gairo, Ditram Wila, ameahidi kuendelea kuboresha huduma kwa walipakodi kwa kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa haki na kwa kuzingatia sheria, sambamba na kuwafuata wafanyabiashara katika maeneo yao kwa ajili ya kuwafanyia makadirio sahihi ya kodi.

Hayo yanajiri baada ya TRA kufanya ziara katika maeneo mbalimbali wilayani Gairo, ambapo walikutana na wafanyabiashara na wananchi katika minada na maeneo ya biashara, kwa lengo la kuwaelimisha umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati na kutoa risiti wanapotoa huduma kwa wateja wao.

Katika ziara hiyo, TRA ilitoa pia zawadi kwa baadhi ya wafanyabiashara na viongozi wa Wilaya ya Gairo, akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya, Jeremia Mapogo, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao na kuimarisha ushirikiano katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...