Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema Mkoa wa Pwani unaendelea kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa vitendo, hususan katika eneo la uzalishaji wa ajira kwa vijana, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Kunenge ametoa kauli hiyo leo Januari 05, 2026, alipofanya ziara ya kutembelea kongani ya viwanda ya Gaini Company Limited iliyopo Kata ya Kikongo wilayani Kibaha mkoani Pwani, ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira zipatazo 1,500 ifikapo mwezi Machi 2026.
Amesema uwekezaji huo unaendana kikamilifu na mkakati wa Serikali wa kukuza uchumi wa viwanda pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, hususan vijana, hatua inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Pwani na kuongeza mapato ya Taifa kwa ujumla.Ameeleza kuwa Mkoa wa Pwani unaendelea kushirikiana na taasisi wezeshi zikiwemo TANESCO, DAWASA na TANROADS, ili kuhakikisha hakuna urasimu wowote katika utekelezaji wa masuala ya uwekezaji. Hatua hiyo inalenga kuwezesha upatikanaji wa mahitaji muhimu ikiwemo nishati ya umeme, maji pamoja na miundombinu ya barabara.
Aidha, ameongeza kuwa mradi wa bomba la gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze tayari umefanyiwa upembuzi yakinifu wa Bilioni 2.3 na TPDC, jambo litakaloongeza ufanisi wa upatikanaji wa nishati kwa viwanda mkoani humo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi katika kongani hiyo QS Bradley Cuthbert Muro, amesema ujenzi wa viwanda viwili umefikia hatua za mwisho, ambapo kiwanda cha chuma kimefikia asilimia 85 ya ujenzi huku kiwanda cha cubes kikifikia asilimia 95. Ameeleza kuwa ifikapo mwezi Machi mwaka huu, uzalishaji utaanza rasmi.
Ameongeza kuwa kongani hiyo itakuwa na viwanda mbalimbali ikiwemo heavy duty industry, medium industry na light duty industry, vikiwemo viwanda vya uzalishaji wa Nondo, Mabati, Steel Pipes, Hallow Sections (RHS) Squqre, Hallow Sections (SHS) Circular, Hallow Sections (CHS) Flat bars pamoja na Misumari.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...