Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza jambo wakati akifungua Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha, ambapo alitumia fursa hiyo kuipongeza Mamlaka hiyo kwa kuendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali baada ya kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 18.77 sawa na ufanisi wa asilimia 103.7 ya lengo lililowekwa la kukusanya shilingi trilioni 18.10.
Naibu Waziri wa Fedha anayeshughulikia Uchumi na Sera, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliofunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (hayupo pichani), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Fedha anayeshughulikia Utawala na Sekta ya Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliofunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (hayupo pichani), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Albina Chuwa, akimkaribisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Hayupo pichani) kufungua Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Watumishi Waandamizi wa Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akifungua Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), akimkabidhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Bw. Hamis Livembe, tuzo ya kupongeza wafanyabiashara katika kusaidia kuvunja rekodi ya ukusanyaji mapato kwa nusu mwaka wa fedha 2025/26, wakati wa Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kufungua Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha. Wengine katika picha ni Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) (wa nne kushoto aliyeketi)na Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (wa tano kushoto aliyeketi), Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Dkt. Albina Chuwa (wa tatu kushoto aliyeketi), Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Yusuph Mwenda (wa tano kulia), Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Bw. Hamis Livembe (kushoto), na viongozi wengine waandamizi wa TRA na Sekta binafsi.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha)

***************

Na. Joseph Mahumi, WF, Arusha

Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (MB), ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, hatua iliyochangia kuimarika kwa uchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Ametoa Pongezi hizo wakati akifungua Mkutano wa Kutathmini Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 (Mid-Year Performance Review Meeting), uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.

Mhe. Balozi Khamis, alisema kuwa Mamlaka hiyo imeendelea kuonesha ufanisi mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ambapo katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 ilikusanya shilingi trilioni 18.77 sawa na ufanisi wa asilimia 103.7 ya lengo la kukusanya trilioni 18.10.

“Mwezi Desemba pekee, TRA mmeweka rekodi mpya kwa kukusanya shilingi trilioni 4.13 kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hii, mafanikio haya ni kiashiria tosha kwamba TRA ipo katika mwelekeo mzuri wa kufanikisha na hata kuvuka lengo la mapato lililopangwa kwa mwaka wa fedha 2025/26. Hongereni sana kwa jitihada zenu,” alisema Mhe. Balozi Khamis.

Aidha, aliongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na sera na miongozo madhubuti inayowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa uwekezaji wa mifumo ambao umeleta mapinduzi katika makusanyo ya kodi.

“Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha uchumi kupitia mageuzi ya mifumo ya mapato, sera bora za kodi na matumizi ya teknolojia za kisasa katika ukusanyaji wa mapato na yameiwezesha TRA kufanya vizuri zaidi mwaka hadi mwaka,” alisema Mhe. Balozi Khamis.

Mhe. Balozi Khamis, aliitaka TRA kuhakikisha Mfumo Mpya wa IDRAS unafanya kazi kwa ufanisi mara tu baada ya kuzinduliwa rasmi, ili kuongeza uwazi, ufanisi na usimamizi bora wa ukusanyaji wa mapato sambamba na kuendelea kupanua wigo wa kodi, hasa katika sekta isiyo rasmi, biashara mtandaoni na uchumi wa kidijitali, pamoja na kutumia mbinu rafiki na zenye kuzingatia utu wa mlipakodi ili kujenga uhusiano wa kuaminiana kati ya TRA na walipakodi.

Kwa upande wao Naibu Mawaziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) na Mhe. Laurent Luswetula, wameahidi kutoa ushirikiano kwa Mhe. Waziri wa Fedha, ili kuhakikisha wanaisimamia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili iweze kuendelea kutimiza malengo yake ya muda mfupi na mrefu ya kukusanya mapato, na kuboresha zaidi uhusiano wake na walipa kodi.

Akizungumza kwa Niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Albina Chuwa, alisema kuwa wataendelea kuhakikisha wanapanua zaidi wigo wa walipa kodi kutoka milioni 7 waliopo hivi sasa hadi milioni 21 ili kuwa na mapato mengi zaidi kusaidia ujenzi wa miradi ya wananchi.

Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Yusuph Mwenda, aliwapongeza wafanyabiashara kwa namna walivyotimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kuwezesha kufikia malengo waliyofikia katika Nusu Mwaka wa Fedha 2025/26.

Bw. Mwenda alisema kuwa kupitia Mkutano huo TRA itatathmini miezi sita ijayo, maeneo ya kuboresha zaidi ili kufikia malengo ya makusanyo ya mapato ifikapo Juni 2026 baada ya TRA imeweza kurekodi Ukuaji chanya wa asilimia 13.6 katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, hali inayoonesha matokeo chanya kwa Mamlaka kusimamia mapato ya Serikali, pamoja na juhudi za Serikali kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.

“Ufanisi wa makusanyo uliofikiwa na TRA kwa miezi ya Julai hadi Desemba 2025 ni kiashiria chanya katika kuhakikisha kuwa lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 la Shilingi trilioni 36.06 linafikiwa” aliongeza Bw. Mwenda

Aliongeza kuwa Mamlaka hiyo imeweka lengo la kuhakikisha sehemu ya makusanyo ya mapato kwenye Pato la Taifa (revenue to GDP ratio) kwa mwaka 2025/26 inakuwa ni zaidi ya asilimia 14.1, toka kwenye kiwango cha asilimia 13.7 kilichorekodiwa mwaka 2024/25 ambapo katika kufanikisha hilo, Menejimenti ya TRA imeendelea kutekeleza kikamilifu mikakati iliyojiwekea, ikiwemo kuhakikisha kuwa Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani Uliohuishwa (IDRAS) unaanza kutumika kuanzia Mwaka huu 2026.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...