
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amewataka wananchi waliokuwa wakitarajia kuwapokea ndugu zao waliokuwa wakisafiri kutoka Mkoa wa Morogoro Desemba 31, 2025 na ambao hadi sasa hawajafanikiwa kuwapata, kujitokeza katika Ofisi za Serikali za Wilaya au Mkoa kutoa taarifa zitakazosaidia zoezi la utambuzi wa miili ya waliofariki dunia katika ajali ya barabarani.
Ajali hiyo ilihusisha basi dogo la abiria la kampuni ya Bill Mawio na lori la mizigo aina ya HOWO, na ilitokea katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Hadi asubuhi ya leo Januari 02, 2026, jumla ya miili 10 imehifadhiwa, ambapo miili minne imetambuliwa kati yake mitatu ni ya wanaume na mmoja ni wa mwanamke. Kati ya miili hiyo, mwili mmoja wa mwanaume ulikuwa umehifadhiwa katika Kituo cha Afya Mikese. Miili sita iliyosalia inaendelea kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba (DNA) ili kubaini utambulisho wao.
Akizungumza leo Januari 02, 2026 alipofika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kuwajulia hali majeruhi waliolazwa, Malima alisema basi la kampuni ya Bill Mawio lilikuwa likitokea Kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani cha Msamvu Morogoro kuelekea Mombo mkoani Tanga, likipitia Mkoa wa Pwani, jambo linaloashiria uwezekano wa baadhi ya abiria kuwa walikuwa wakitarajia kushuka njiani katika mikoa jirani.
“Kwa kuwa gari lilianzia hapa Morogoro, tunawaomba ndugu ambao wapendwa wao waliwaaga wakisafiri kuelekea maeneo hayo na hadi sasa hawajulikani walipo, wafike Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi. Serikali ya Mkoa itagharamia huduma zote zitakazohitajika,” alisema Malima.
Akitoa taarifa ya hali za majeruhi, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Joseph Kway, alisema hadi Januari 01, 2026 mgonjwa mmoja alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na jeraha kubwa lililokuwa likihatarisha kupoteza mguu, baada ya kushauriana na mgonjwa pamoja na ndugu zake.
Dk. Kway alisema wagonjwa watano wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya jopo la madaktari kujiridhisha kuwa hali zao ni nzuri. Hadi Januari 02, 2026, hospitali imeendelea kuwahudumia majeruhi 17 wakiwemo wanaume tisa na wanawake wanane, kati yao watoto wanne. Aliongeza kuwa hali zao kwa ujumla ni nzuri, ingawa mgonjwa mmoja anatarajiwa kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na changamoto ya kuvunjika mfupa wa nyonga.
Kuhusu waliopoteza maisha, Dk. Kway alisema timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali tayari imewasili na kuchukua sampuli sita za vinasaba kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara, zikiwemo sampuli nne za wanaume na mbili za wanawake. Hadi sasa, ndugu mmoja pekee ndiye aliyejitokeza kwa ajili ya vipimo vya DNA, huku miili mitano bado ikisubiri ndugu zao kujitokeza.
Ajali hiyo ilitokea jioni ya Desemba 31, 2025 na kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, chanzo chake ni uzembe wa dereva wa lori aliyekuwa akijaribu kuyapita magari mengine bila tahadhari wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha. Hali hiyo ilisababisha magari hayo kugongana uso kwa uso na kisha kuteketea kwa moto eneo la tukio.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...