Wakazi wa Majengo na Amani Mbezi kwa Msuguli wakiwa wamepanga foleni kuchota maji kwa mmoja ya mwananchi wa mtaa wa pili.

Dar es Salaam Januari 6, 2025: Wakazi wa mitaa ya Majengo na Amani iliyopo Mbezi kwa Msuguli, wameilalamikia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kile walichokitaja kuwa manyanyaso na uzembe wa muda mrefu katika utoaji wa huduma ya maji, hali iliyosababisha maisha yao kuwa magumu kwa kipindi kirefu.

Wakizungumza katika kikao chao cha Mtaa kilichofanyika hivi karibuni, wakazi hao wamesema wamekuwa hawapati maji kwa muda mrefu licha ya kuwepo kwa ratiba ya mgao wa maji iliyotolewa na DAWASA yenyewe, ratiba ambayo kwao haijawahi kutekelezwa ipasavyo.

Mmoja wa wakazi hao, Mama Rhoda, alisema hali ya upatikanaji wa maji katika Mtaa wa Majengo ni ya kusikitisha huku akishangazwa na ukweli kwamba mitaa ya jirani kama Masaki, Malamba Mawili na Kanisa la Udongo inayohudumiwa na kituo cha Kimara imekuwa ikipata maji kwa uhakika.


“Sisi wakazi wa Majengo tumekuwa tukipata maji kwa shida sana. Tunajiuliza, kwa nini sisi tu? Wenzetu wa Masaki na Kanisa la Udongo wanapata maji, yanatoka wapi? Sisi tunaohudumiwa na Kinyerezi kila siku ni hadithi tu,” alisema Mama Rhoda.

Naye Albert Mwemezi alisema DAWASA Kinyerezi imekuwa ikitoa ahadi hewa kwa kudai maji yatatoka siku za Alhamisi, Jumapili na Jumatatu, lakini hakuna utekelezaji zaidi ya maneno ya “kesho”.


Kwa upande wake, Ngosha Jacob, mteja mkubwa wa DAWASA katika eneo hilo anayefyatua matofali alisema upungufu wa maji umeathiri moja kwa moja shughuli za uzalishaji licha ya wao kulipa bili kwa wakati.

“Huduma ya maji ni muhimu sana kwa shughuli zetu za uzalishaji. Inashangaza tunalipa bili kwa wakati lakini huduma hatupati. Huu ni uzembe mkubwa,” alisema Jacob.

Mkazi mwingine, Abdul Shaban, alisema miezi miwili iliyopita aliwasiliana moja kwa moja na Mkurugenzi Mkuu wa DAWASA ambaye alikiri kupokea malalamiko yao na kuahidi kuyafanyia kazi, hata hivyo juhudi hizo hazikuzaa matunda kwani kero hiyo bado haijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Licha ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kuweka kambi katika eneo la Kinyerezi, wakazi wa Majengo na Amani wamesema wamekaa bila maji kwa zaidi ya miezi mitatu hadi minne, hali inayowaacha katika mateso makubwa.

Mkazi mmoja aliyeomba kutotajwa jina lake alisema maji yamekuwa anasa, na kwa sasa wanalazimika kununua maji kwa mkazi mwenye kisima kwa gharama ya shilingi 500 kwa dumu moja.

Mwandishi wa MMG aliyefika eneo la tukio na kujionea hali halisi ya maisha ya wakazi hao, alijaribu kuwasiliana na uongozi wa DAWASA upande wa Kinyerezi lakini hakupata majibu ya moja kwa moja zaidi ya ahadi za “maji yatatoka kesho”.

Wakazi wamesisitiza kuwa kero yao ya maji ilikuwepo hata kabla ya tangazo la mgao wa maji lililotolewa na Waziri wa Maji, wakitaka DAWASA kutoitumia hoja ya uhaba wa maji kama kisingizio.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi, Ayoub Rusungu alisema kuna mitaa ya jirani inayopata maji angalau mara mbili kwa wiki, jambo linaloibua maswali juu ya usawa na haki katika utoaji wa huduma.

“Kwa nini mitaa mingine ipate maji mara kwa mara halafu sisi tusipate hata mara moja kwa wiki? Hapa kuna jambo halipo sawa. Kuna mitaa yenye watu wakubwa wanapata maji, sisi wanyonge tunaachwa bila maji kabisa,” alisema Rusungu.

Wakazi hao wametoa wito kwa DAWASA na Wizara ya Maji kuingilia kati kwa haraka ili kutatua kero hiyo ya muda mrefu, wakisema maji ni huduma ya msingi na haki yao ya msingi kama wananchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...