-Aonya watendaji wa Serikali “kuzoea” matatizo ya wananchi
-Azindua mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa anataka kuona kila fedha inayotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo inatumika kama ilivyokusudiwa.
Amesema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wa Serikali wenye dhamana wanashindwa kufuatilia matumizi ya fedha na kusababisha kushindwa kutekelezwa kwa miradi kwa viwango na ubora kwa manufaa ya wananchi.
Amesema hayo leo Jumanne (Februari 17, 2026) alipokuwa anazungumza na wananchi baada ya kuzindua mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Mradi huo ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 526.8 una uwezo wa kuzalisha mitungi 120 ya kilo 50 kwa siku, hivyo kuboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma hii muhimu.
Mitambo hiyo imeiwezesha Halmashauri kutolazimika kusafirisha mitungi ya oksijeni hadi Jijini Tanga umbali wa takribani kilometa 175 kwa ajili ya ujazaji. Hadi sasa, mtambo umefanikiwa kuzalisha mitungi 1,440 ya hewa tiba (oksijeni) ya kilo 50 na Mitungi 200 ya kilo 15.
Aidha, Waziri Mkuu amewasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha kutekeleza majukumu yao ipasavyo na si vinginevyo. “Tunataka watu wasilale ofisini, ninyi ni watumishi wa Serikali, fedha zikiletwa zikafanye kazi iliyokusudiwa.”
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema hayo wakati akihoji kuhusu kukosekana kwa ubora na viwango vya majengo, risiti za malipo, kutofanyika kwa kodi ya zuio, kukosekana kwa cheti cha ubora wa mabati, matofali na saruji katika baadhi ya shule za msingi wilayani humo.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameonya tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuwa na utaratibu wa kuzoea matatizo ya wananchi. “Wapo baadhi ya watendaji wa Serikali wanapokea matatizo ya wananchi kama salamu na badala yake matatizo yanalimbikizwa sana.”






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...