Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amewataka waajiri kuhakikisha kila muajiriwa anakuwa na uhakika wa matibabu kuelekea utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Dkt. Magembe amesema hayo leo Machi 10, 2026 baada ya wasilisho la maandalizi ya Bima ya Afya kwa Wote kwenye mkutano na Wakurugenzi Wakuu wa Makampuni ya Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania – CEOrt) uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha viongozi kutoka serikalini, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

"Serikali inaendelea kuimarisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuwa na ubunifu wa vyanzo vya fedha pamoja na kuanzisha kitita muhimu kitakachohakikisha kila mwananchi anapata huduma muhimu za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma nchini," amesema Dkt. Magembe

Aidha, Dkt. Magembe amesema Serikali imeanza utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambapo utekelezaji wake unafanyika kwa awamu, awamu ya kwanza ilianza Januari 6, 2025 kwa kuwatambua zaidi ya familia milioni 3.6 kidijitali kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa," amesema Dkt. Magembe

Katika hatua nyingine, Dkt. Magembe amesema Serikali imeanzisha Mfuko wa kugharamia huduma za Afya (Health Equity Fund) utakaosaidia kugharamia huduma za afya kwa wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu kupitia vyanzo mbalimbali.

Pia, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kupunguza utegemezi wa misaada ya wahisani katika sekta ya afya kwa kuimarisha zaidi vyanzo vya ndani vya fedha na kutafuta mbinu mpya za ubunifu zitakazochangia kugharamia huduma za afya nchini.

Hata hivyo, ameeleza dhamira ya Serikali kuimarisha viwanda vya ndani vya dawa na bidhaa za afya ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa unakuwa wa uhakika, kuongeza ajira na kukuza sekta binafsi kuelekea utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.

Mwisho, Serikali imewahimiza wawekezaji kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo, huku ikiendelea kukuza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...