Na Emmanuel Mbatilo, Kibaha

Wananchi wa Kijiji cha Kitomondo, wilayani Kibaha mkoani Pwani, wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kati yao na mfugaji anayedaiwa kumiliki eneo la takribani hekari 7,000.

Eneo hilo linaelezwa kuenea hadi wilaya jirani ya Kisarawe na kusababisha wananchi kukosa maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ikiwemo kilimo.

Wananchi hao wamesema mgogoro huo umeathiri maisha yao kwa kiasi kikubwa, huku wakidai kuwa umewanyima fursa ya kujiletea maendeleo kupitia matumizi ya ardhi.

Kwa upande wao, wananchi wameisisitiza Serikali kuingilia kati haraka ili kumaliza sintofahamu iliyopo, wakieleza kuwa kuchelewa kwa suluhisho kunazidi kuathiri ustawi wa kijiji hicho.

Akizungumza kwa njia ya simu Machi 22, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, amesema tayari timu ya wataalamu imefanya uhakiki wa mipaka na kubaini kuwa chanzo kikuu cha mgogoro huo ni uuzaji holela wa ardhi.

Amesema baada ya suala hilo kufikishwa ofisini kwake, alipendekeza njia mbili za kutatua mgogoro huo, ambazo ni kufikia maridhiano kati ya pande husika au kufungua kesi katika Mahakama ya Ardhi ili kupata ufafanuzi wa kisheria.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitomondo, Ramadhani Kiluka, amesema kuchelewa kwa utatuzi wa mgogoro huo kunaweza kusababisha wananchi kupoteza imani kwa Serikali.

Amesema kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, hali hiyo inaweza kuendelea kudhoofisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...