•Zilifichwa zenye mfumo wa AC na maeneo mengine ya basi hilo

*Ni basi linalofanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 101.2 katika la Tabata Kibo jijini Dar es Salaam zikiwa zimefichwa katika basi la abiria aina ya Yutong la kampuni ya Abood lenye namba ya usajili T 181 EMJ lililokuwa likifanya safari kati ya Mombasa, Kenya na Dar es Salaam, Tanzania.

Akizungumza leo Aprili 14,2026 Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) Aretas Lyimo amesema dawa hizo zilifichwa katika maeneo mbalimbali ya basi hilo ikiwemo ndani ya mfumo wa hewa (AC) kwa lengo la kukwepa kugundulika.

Kamishina Jenerali Lyimo amesema watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni dereva wa basi Ramadhan Mohamed (52), Salma Sanga (26) kondakta, Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39). Mkoani Pwani kilogramu 419.09 za mirungi zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa kuelekea Dar es Salaam.

Akifafanua kuhusu tukio hilo amesema kwa mujibu wa sheria wanaotakiwa kukamatwa ni wale ambao wanatuhumiwa kukutwa na dawa za kulevya lakini kwa kuwa waliokutwa ni dereva na kondakta ndio maana ba basi hilo nalo linashikiliwa na mamlaka hiyo kwa hatua nyingine za kisheria.

Akitoa taarifa kuhusu operesheni iliyofanywa na mamlaka hiyo katika maeneo mbalimbali nchini amesema DCEA) imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa mbalimbali za kulevya, kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu, vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.

Sambamba na ukamataji huo, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku watuhumiwa 77 wakikamatwa kuhusiana na makosa hayo. Katika matukio hayo, magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vilikamatwa.

Akifafanua amesema uchambuzi wa takwimu umebaini ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya aina ya mirungi, ambapo kilogramu 1,267.12 zilikamatwa, sawa na 64 ya dawa zote zilizokamatwa mwezi huo.

“Hali hii imetokana na mkakati wa Mamlaka kujikita katika operesheni za dawa za kulevya za mashambani baada ya kudhibiti kwa kiasi kikubwa mitandao ya dawa za kulevya za viwandani.Baadhi ya matukio ya ukamataji yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.” Amesema Kamishna Jenerali Lyimo

Miongoni mwa matukio hayo amesema katika Mkoa wa Mwanza zilikamatwa kilogramu 52 za mirungi katika kizuizi cha barabarani cha Magu pamoja na Bandari ya Mwanza South, ikisafirishwa kwa kutumia gari aina ya Fuso yenye namba ya usajili T 296 APA.

Amesema dawa hizo zilikuwa zimefichwa katikati ya mizigo mingine, ikiwemo mabelo ya nguo za mitumba. Dereva wa gari hilo, Hassan Hassan (37), mkazi wa Mahina Nyamagana alikamatwa.

Aidha, wilayani Misungwi mkoani humo, kilogramu 184.9 za mirungi zilikamatwa zikiwahusisha watuhumiwa Chrispin Shoo (62) na mkewe Esther Pastory (55). Dawa hizo zilibainika ndani ya nyumba na katika vyombo vya usafiri ambavyo ni Gari aina ya Toyota Crown yenye namba ya usajili T 742 EGL, Toyota Wish yenye 2 namba ya usajili T 854 DXB, pamoja na bajaji yenye namba za usajili MC 261 EZV.

Pia amesema mkoani Tanga, zilikamatwa Kilogramu 32.95 za Mirungi ikiwa imefichwa ndani ya mfuko kwa kuchanganywa na maembe. Katika tukio hilo, Seif Omar (38), maarufu kwa jina la Haniwao, mkazi wa Mtaa wa Taifa Barabara ya 13, ambaye pia ni mjumbe wa Serikali ya Mtaa alikamatwa.

Katika operesheni nyingine zilizofanyika mkoani humo, jumla ya Kilogramu 164.01 za Mirungi zilikamatwa katika matukio tofauti.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...