Utafiti mpya uliozinduliwa katika Kongamano la Feminist Conversation Space umebaini uwepo wa changamoto kubwa za ufadhili zinazowakabili wasichana na wanaharakati wa masuala ya wanawake (young feminists) katika ukanda wa Afrika Mashariki, hali inayodhoofisha utekelezaji wa shughuli zao licha ya mchango wao mkubwa katika jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, mwakilishi wa Msichana Initiative Consolata Chikoti alisema kuwa licha ya wanaharakati hao kuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko katika masuala mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, afya ya uzazi na haki za kiuchumi, bado wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa rasilimali za kifedha. Utafiti huo umeonesha kuwa ukosefu wa ufadhili wa uhakika ni changamoto namba moja, huku mashirika mengi yakishindwa kulipa watumishi, kuendesha miradi au hata kugharamia shughuli za msingi.

Kwa mujibu wa utafiti huo, fedha zinazopatikana mara nyingi huwa za muda mfupi, zisizo endelevu na hazitoshelezi mahitaji, huku baadhi ya ufadhili ukidumu kwa miezi michache tu. Mashirika ya ngazi ya chini na yale ya vijijini yameonekana kuathirika zaidi kutokana na changamoto za kidijitali pamoja na kushindwa kukidhi masharti magumu ya wafadhili kama vile ukaguzi wa hesabu na miundo rasmi ya taasisi.

Takwimu zinaonesha kuwa nchini Kenya, ni asilimia 38 tu ya mashirika yanayopata ufadhili wa ndani na wa kimataifa kwa pamoja, wakati asilimia 33 yanategemea ufadhili wa ndani pekee ambao mara nyingi huwa mdogo.

Aidha, katika ukanda mzima, baadhi ya makundi hasa yanayoshughulikia masuala ya pembezoni hupata chini ya dola 1,000 kwa mwaka licha ya jukumu lao kubwa katika kushughulikia changamoto za kijamii.

Mbali na changamoto za kifedha, utafiti huo pia umebainisha kuwepo kwa vikwazo vya kijamii na kiusalama, ikiwemo upinzani kutoka kwa jamii, vitisho, unyanyasaji wa mtandaoni pamoja na ukosefu wa huduma za afya ya akili kwa wanaharakati hao.

Hata hivyo, wadau wameeleza kuwa pamoja na changamoto hizo, wanaharakati wa kike wameendelea kuonesha uimara kwa kuandaa na kuendesha harakati katika maeneo mbalimbali kwa rasilimali chache lakini kwa dhamira kubwa.

Katika hatua nyingine, uzinduzi huo uliambatana na kutambulishwa kwa Mfuko wa Wasichana na Wanaharakati wa Kike Afrika Mashariki (East African Girls and Young Feminist Fund), unaolenga kubadili mfumo wa ufadhili kwa kuzingatia uaminifu, kusaidia uongozi wa ngazi ya chini na kuleta mageuzi katika utoaji wa rasilimali.

Washiriki wa kongamano hilo walisisitiza umuhimu wa majukwaa ya majadiliano kama Feminist Conversation Space katika kujenga mshikamano, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mikakati ya pamoja miongoni mwa wanaharakati.

Licha ya changamoto zilizopo, matumaini yameendelea kuwepo, huku wadau wakisisitiza kuwa mshikamano na juhudi za pamoja ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha harakati za usawa wa kijinsia zinaendelea kukua na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...