Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya watu kupinga hatua za Serikali, hasa pale maamuzi hayo yanapogusa maslahi yao binafsi—hususan kwa wale waliokuwa wakinufaika kwa njia zisizo halali.
Akizungumza leo jijini Dodoma mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo yenye urefu wa kilomita 76, pamoja na kipande cha barabara ya Chololo–Mapinduzi (Makao Makuu ya TPDF) chenye kilomita 5, Dkt. Mwigulu alisema Serikali haitayumbishwa na kelele za wachache wanaopinga mabadiliko yenye manufaa kwa taifa.
Alieleza kuwa mara nyingi watu wanaoguswa na hatua hizo hujipanga kwa kuajiri wengine ili kuishambulia Serikali na viongozi wake kupitia mitandao au majukwaa mbalimbali ya kijamii.
“Watanzania msitishike na hao watu, kwa sababu wanafugwa huko waliko. Ili mikataba yao iendelee, ni lazima waendelee kutukana,” alisisitiza.
Dkt. Mwigulu amesema kuwa mwenendo huo si wa sasa pekee, bali umekuwepo hata katika awamu zilizopita za uongozi, ambapo baadhi ya watu walikuwa wakitoa kauli za kejeli na mashambulizi dhidi ya viongozi wanaochukua hatua thabiti.
Aidha, amebainisha kuwa hata yeye binafsi amekuwa mhanga wa mashambulizi hayo, akifananisha hali hiyo na mapambano ya kiimani, ambapo wanaosimama kupinga maovu hukumbana na upinzani mkali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa juhudi za Serikali ya awamu ya sita zinalenga kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi wote.
Amesisitiza kuwa miradi ya maendeleo kama ujenzi wa barabara hizo ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha miundombinu na kukuza uchumi wa nchi.




.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...