Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

BANK of Africa Tanzania imezindua programu ya masuluhisho na huduma mahususi za kifedha pamoja na ushauri kwa Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati (SMEs), ikiwa ni jitihada za kuboresha upatikanaji wa mikopo, elimu ya biashara na kukuza ushindani wa biashara nchini.

Uzinduzi wa programu hiyo ulipongezwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, aliyesema kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha mahitaji ya kifedha ya wajasiriamali kupitia huduma, mikopo na elimu ya biashara.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Tawi la Lumumba jijini Dar es Salaam, Tutuba alisema tukio hilo linaashiria hatua muhimu katika kuimarisha masuluhisho ya kifedha kwa SMEs na kukuza sekta binafsi.

“Mpango huu unaonyesha mabadiliko chanya katika sekta ya benki, kutoka mfumo wa ukopeshaji wa jumla kwenda kwenye huduma jumuishi za kifedha zinazolenga mahitaji maalum ya wateja,” alisema.

Aliongeza kuwa SMEs ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, zikichangia takribani asilimia 95 ya biashara zote na asilimia 35 ya Pato la Taifa (GDP), huku zikitoa ajira kwa zaidi ya watu milioni tano.

Aidha, alisema mpango huo unaendana na Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (2023–2028) unaolenga kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za kifedha nafuu na za kuaminika. Alitaja makundi ya kipaumbele kuwa ni pamoja na wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, wakulima na wavuvi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania, Esther Cecil Maruma, alisema mkakati huo umejengwa katika uelewa wa kina wa mahitaji ya SMEs.

“Tunataka kuwezesha biashara kukua kwa kasi, kushindana vyema na kudumu kwa muda mrefu kupitia masuluhisho yanayojibu changamoto zao moja kwa moja,” alisema.

Alieleza kuwa huduma mpya zilizozinduliwa ni pamoja na ufadhili wa ankara (invoice discounting), overdraft, mikopo ya muda mfupi na mrefu, ufadhili wa mali na magari, dhamana, pamoja na huduma za biashara za kimataifa.

Maruma alisisitiza kuwa benki inalenga kuwa mshirika wa kweli wa ukuaji wa biashara, si mtoaji wa mikopo pekee.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji – Biashara, Hamza Cherkaoui, alisema wameboresha huduma ili ziwe rahisi, zenye unyumbufu na zinazoendana na mahitaji halisi ya biashara.

Naye Mjumbe wa Bodi, Waziri Kindamba, aliipongeza benki hiyo kwa ubunifu huo unaolenga kutatua changamoto za wajasiriamali.

Kwa upande wake, mteja wa muda mrefu wa benki hiyo, Mohammed Bahasawan, alisema mpango huo ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara kukuza mitaji na biashara zao.

“Nimekuwa mteja wa benki hii kwa miaka mingi, na ninaamini huu ni mwanzo wa suluhisho la changamoto nyingi za wajasiriamali nchini,” alisema.
Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba (katikati), akikata utepe kuzindua Programu ya masuluhisho na huduma mahususi za kifedha na ushauri kwa wafanyabiashara wa kati na wadogo (SMEs)wa Bank of Africa, jijini Dar es Salaam juzi. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji - Bank of Africa, Esther Cecil Maruma, Mjumbe wa Bodi - Bank of Africa - Mkurugenzi, Waziri Kindamba (kulia), Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Biashara wa benki hiyo, Hamza Cherkaoui (kushoto) na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uendeshaji wa Bank of Africa, Wasia Mushi.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha SME wa Bank of Africa, Beatrice Richard, akielezea jambo kwa Mgeni rasimi, Gavana wa Emmanuel Tutupa na Viongozi wa benki hiyo, alipotembelea eneo jipya maalum kwa wateja wa SME wakati wa uzinduzi juzi.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutupa na Mjumbe wa Bodi wa Bank of Africa, Waziri Kindamba na Mkurugenzi Mtendaji - Bank of Africa, Esther Cecil Maruma (kulia walio kaa) wakiwa katika picha ya pamoja na wateja wa benki hiyo, wakati wa uzinduzi wa masuluhisho na huduma mahususi za kifedha na ushauri kwa Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati (SMEs).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...