Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), leo 21 Aprili 2026, imetumia fursa ya Wiki ya Nishati kuwahamasisha waheshimiwa wabunge kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya mafuta maeneo ya vijijini pamoja na vituo vya CNG ili kuendelea kusogeza huduma kwa wananchi.

Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Wilfred Mwakalosi, alisema kuwa EWURA inatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu namna inavyohakikisha upatikanaji wa huduma za nishati na maji kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Alibainisha kuwa wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hivyo kuwajengea uelewa kuhusu udhibiti, fursa za uwekezaji na utaratibu wa kupokea na kushughulikia migogoro na malalamiko kutawawezesha kuwasilisha taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu juhudi za Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za umeme, mafuta na gesi asilia.

Akizungumza katika maonesho hayo, Ofisa Mwandamizi wa Kitengo cha Mafuta, Mha. Ibrahim Kajugusi, alisema elimu inayotolewa pia inalenga kuwafahamisha wananchi jinsi EWURA inavyosimamia upatikanaji wa huduma za mafuta nchini kwa kuzingatia ubora uliopitishwa na gharama sahihi. Aidha, aliwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta hiyo, hususan ujenzi wa vituo vya mafuta vya gharama nafuu vijijini na mijini pamoja vituo vya kujazia gesi asilia kwenye magari (CNG).

Kwa upande wake, Bi. Achilana Mtingele, mchumi wa EWURA, alisema elimu inayotolewa imejikita katika kueleza namna EWURA inavyosimamia upangaji wa viwango vya bei za huduma za umeme, mafuta na gesi asilia. Aliongeza kuwa mamlaka hiyo huweka mizania kati ya maslahi ya watoa huduma na watumiaji, na kwamba wabunge waliopata elimu hiyo wataweza kuiwasilisha ipasavyo kwa wananchi katika maeneo yao.

Akizungumzia sekta ya gesi asilia, Mhandisi Mwandamizi wa Gesi Asilia, Mha. Evaline Rweikiza, alisema EWURA itaendelea kusimamia ubora wa miundombinu ya gesi asilia nchini na kuhamasisha matumizi yake, hususan katika magari. Alibainisha kuwa hadi sasa vituo 18 vimepata leseni ya EWURA kutoa huduma ya gesi asilia, huku vituo sita vingine vikiwa katika hatua za mwisho za kupata leseni katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Aidha, mipango inaendelea kwa baadhi ya makampuni kusambaza gesi asilia iliyokandamizwa katika mikoa ya Morogoro na Dodoma.

Kwa upande wa sekta ya umeme, Mhandisi Mwandamizi wa Umeme, Lulu Chilumba, aliwahamasisha wabunge na wadau wanaotembelea maonesho hayo kutumia mafundi umeme wenye leseni kutoka EWURA ili kuhakikisha usalama wa nyumba na mali zao. Alisema EWURA inaendelea kutoa leseni kwa mafundi umeme wenye sifa stahiki, ambapo zaidi ya leseni 1,000 zilitolewa katika mwaka wa fedha uliopita.

Naye Ofisa Rasilimali Watu Mkuu, Bi. Limi Kahabi, alisema EWURA ni mwajiri anayezingatia misingi ya usawa na haki katika mchakato wa ajira, akisisitiza kuwa taasisi hiyo huajiri kwa kuzingatia sifa, weledi na usawa kwa wote.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...