Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze, Aprili 19, 2026
MWENGE wa Uhuru umetambua mchango wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, kufuatia kuandika kitabu(andiko) kinachoelezea falsafa ya Mwenge wa Uhuru tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961.
Imeelezwa Juhudi hizo za Ridhiwani, amezifanya wakati alipokuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, kuandika andiko hilo rasmi Kiserikali.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, alitambua mchango huo kuwa sehemu ya historia ya Taifa wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika Aprili 19, 2026 katika Shule ya Msingi Kiwangwa, Halmashauri ya Chalinze, ukitokea Halmashauri ya Bagamoyo.
Mbali ya hilo, Ridhiwani ametajwa kuwa miongoni mwa wananchi wawili wa wilayani Bagamoyo waliotoa mchango wa kipekee kwa jamii, ambapo mmoja alijitolea kuvusha watoto darajani kwenda shule, huku mwingine akitoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Mwang'onda alieleza, Mwenge wa Uhuru ni moja ya tunu kubwa za Taifa, ukiwa kichocheo muhimu cha maendeleo, hususan katika kupambana na ujinga, maradhi na umaskini.
Awali, akipokea Mwenge huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Ramadhan Possi, alieleza jumla ya miradi saba yenye thamani ya sh. bilioni 34.179 inapitiwa, ambapo miradi mitatu imezinduliwa, mitatu imekaguliwa na mmoja umetembelewa.
Wakati huohuo, Mwang’onda ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Kituo cha Afya Kiwangwa uliogharimu shilingi milioni 20.583.
Pia Mwenge wa Uhuru umetembelea ujenzi wa boksi kalvati katika barabara ya Mwinyi–Kudiembe, Kata ya Bwilingu, uliotekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 67.3 kupitia TARURA; na kutembelea kiwanda cha Starlinkgulf Trading Co. Ltd (Wallput) kilichojengwa kwa gharama ya zaidi ya sh bilioni 34.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...