Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Manyoni

HOSPITALI ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida imesema hospitali hiyo kwa sasa imekuwa na uwezo mkubwa wa utoaji bora wa huduma za afya kutokana na uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kisasa vilivyotolewa na Bohari ya Dawa(MSD).

Kwa mujibu wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni ni kwamba MSD wamepeleka vifaa vya kisasa ambavyo vimewezesha kurahisisha huduma kwa wateja(wagonjwa) ikiwemo mashine yenye uwezo wa kupima sampuli nane kwa wakati mmoja hali ambayo pia imesaidia kupunguza msongamano.

Akizungumza katika ziara ya kikazi iliyoandaliwa na MSD ya kutembelea hospitali hiyo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida Dk.Bwire Robert amesema MSD wamefanya mageuzi makubwa ya kiutendaji katika usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali, vituo vya afya na Zahanati nchini. 

Amesisitiza mabadiliko yaliofanywa na MSD yamewarahisishia wao kama watoa huduma za afya kwa wananchi kufanyakazi zao kwa kujiamini huku malalamiko ya wananchi kuhusu huduma yakipungua kwa kiasi kikubwa.

Dk.Bwire kwa sasa MSD wanafanyakazi kidijitali jambo ambalo linarahisisha mpaka ngazi ya kijiji kutoa oda ya dawa na kufanyiwa kazi ndani ya muda mfupi na hatimaye kupata dawa na vifaa tiba. 

“Kumekuwa na mapinduzi makubwa katika utoaji huduma kutokana na Serikali kuwekeza katika vifaa tiba,  dawa na watoa huduma.”

Akieleza zaidi Dk.Bwire amesema uamuzi wa MSD kuwezesha uwepo wa chumba maalum na vifaa tiba kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti umewezesha sasa watoto hao kuhudumiwa vema na kukua bila changamoto yeyote na kusisitiza hivi sasa hata mtoto mwenye gramu 600 wana uhakika atahudumiwa,atakuwa salama.

“MSD imetuletea vifaa maalum vya kuwatunzia watoto njiti na uwepo wa vifaa hivyo tumepunguza vifo vya watoto njiti kwa asilimia 90,haya ni mafanikio makubwa sana katika sekta ya afya.Tunaipongeza Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia kwani kupitia MSD huduma za afya zimekuwa bora na za uhakika.”

Pamoja na hayo amesema pia MSD imewezesha hospitali ya Wilaya ya Hospitali Manyoni kuwa na vifaa vya maabara vya kisasa ikiwemo mashine za UtraSound ya kisasa, mashine za upasuaji, na Mashine ya usingizi . 

Kuhusu vitanda vyenye mashine za kupumulia amesema wanavyo vya kutosha hivyo kwao sio changamoto tena huku akieleza kuwa uamuzi wa MSD kujenga chumba cha kisasa cha kuhifadhia maiti imesaidia miili ya wapendwa wetu kuhifadhiwa sehemu salama katika hospitali hiyo.

Awali Meneja MSD kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa amefafanua kwamba MSD inahudumia  vituo zaidi ya 400 kwa Mkoa wa Singida huku Kanda Nzima ya Kati ikiwemo Mkoa wa Singida, Dodoma na Wilaya ya Kiteto ikiwa na jumla ya vituo zaidi ya 840.

Kwa wa upande wa wananchi wa Wilaya ya Manyoni wameipongeza Serikali kupitia MSD kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kuiwezesha Hospitali ya Wilaya kuwa na vifaa tiba vya kisasa sambamba na uhakika wa dawa kwani yale malalamiko ya kukosa huduma hayapo tena.

Wananchi hao walipoulizwa kuhudumiwa katika hospitali za serikali au binafsi wanachagua kwenda wapi wamejibu kwa sasa kimbilio lao ni katika hospitali za serikali kwani hakuna huduma ambayo wanaihitaji wameikosa kwa kuwa kuna kila kitu.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...