Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesisitiza kuwa uendelevu wa Taifa hauwezi kupatikana iwapo wananchi hawatazingatia utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa changamoto za mabadiliko ya tabia nchi zinaweza kuathiri ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, katika maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Shule ya Msingi NaneNane, kata ya Nzuguni, Shekimweri amesema ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira ili kukabiliana na athari kama ukame.
Katika kuadhimisha Muungano huo, Shekimweri alishiriki zoezi la upandaji miti katika Shule ya Msingi NaneNane, ambapo jumla ya miti 162 imepandwa, ameeleza kuwa idadi hiyo inaashiria miaka ya Muungano na umoja wa Taifa, Aidha, amewataka wanafunzi na walimu kuitunza miti hiyo ili iweze kukua na kuleta manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Sambamba na hilo, amewataka wananchi kuendelea kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano ulioasisiwa na waasisi wa Taifa la Tanzania, Amesema misingi hiyo inapaswa kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, familia, jamii hadi Taifa kwa ujumla.
Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 62 ya Muungano, nchi imepiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya na usafirishaji. Amesema huduma za afya sasa zinapatikana hadi ngazi ya kata kutokana na upatikanaji wa vifaa tiba, hali iliyopunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Kwa upande wa usafirishaji, amesema maboresho yaliyofanyika yamerahisisha safari, ambapo kwa sasa inawezekana kusafiri kutoka Dodoma kwenda Zanzibar na kurejea siku hiyo hiyo, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yalianza Aprili 24, 2026 kwa shughuli mbalimbali ikiwemo usafi kwenye kata zote, mdahalo, maandamano ya amani ya kilomita 6.2 na bonanza la michezo, kabla ya kuhitimishwa Aprili 26, 2026 kwa zoezi la upandaji miti.






.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...