Na Mwamvua Mwinyi, Pwani, April 16, 2026
MKOA wa Pwani umejipanga kupokea Mwenge wa Uhuru Aprili 18, 2026, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi katika Shule ya Msingi Mtambani, Kata ya Mapinga, wilayani Bagamoyo, ambapo mwenge huo utapokelewa ukitokea Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu ujio wa Mwenge wa Uhuru, alieleza mwenge utakagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ndani ya halmashauri tisa zilizopo katika wilaya saba.

“Sisi tumejipanga kama tulivyofanya vizuri mwaka uliopita, na mwaka huu kama kawaida yetu tumeweka miradi inayogusa maslahi ya wananchi. Haturudii miradi, na tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alifafanua Kunenge.

Aliongeza kuwa mwaka uliopita mkoa huo ulipata jukumu la kuwasha Mwenge wa Uhuru kitaifa na ulifanya vizuri kwa kushika nafasi ya kwanza.

Aidha, katika tathmini ya halmashauri 184 za Tanzania Bara na Zanzibar, Chalinze ilishika nafasi ya pili, Manispaa ya Kibaha nafasi ya tatu, Bagamoyo nafasi ya tisa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha nafasi ya 11.

Kunenge alibainisha kuwa,lengo la Mbio za Mwenge wa Uhuru ni kuimarisha umoja, mshikamano na udugu miongoni mwa Watanzania.

Alieleza baada ya kupokelewa, Aprili 18 utapokelewa na kukimbizwa halmashauri ya Bagamoyo, Aprili 19 Chalinze, Aprili 20 Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Aprili 21 Manispaa ya Kibaha, Aprili 22 Mafia, Aprili 23 Kisarawe, Aprili 24 Mkuranga, Aprili 25 Kibiti, Aprili 26 Rufiji na Aprili 27 utakabidhiwa mkoani Lindi.

Kwa mwaka 2026, Mwenge wa Uhuru umebeba ujumbe wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa chini ya kauli mbiu isemayo: “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”

Vilevile mbio hizo pia hubeba jumbe za kudumu zikiwemo kuimarisha mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, dawa za kulevya, lishe bora na vita dhidi ya rushwa.

Kutokana na umuhimu huo, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za Mwenge wa Uhuru katika wilaya zote utakazopitia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...