Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wanawake na vijana barani Afrika kuongeza juhudi, kujituma na kujiamini katika ndoto zao ili kufanikisha maendeleo ya binafsi na ya kijamii.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Aprili 11, 2026, mara baada ya kutunukiwa shahada ya heshima na Chuo Kikuu cha Nasarawa, tukio ambalo limebeba heshima kubwa kwa uongozi wake na mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Rais Samia amesema safari yake ya uongozi ni ushahidi tosha kwamba mafanikio yanawezekana hata pale mtu anapokutana na changamoto mbalimbali za maisha, mradi tu awe na bidii, ujasiri na maono ya mbali.
Amebainisha kuwa Serikali na yeye binafsi wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, elimu na sekta ya uchumi, akisisitiza kuwa hakuna jamii inayoweza kufikia maendeleo kamili iwapo nusu ya nguvu kazi (wanawake) haitashirikishwa kikamilifu.
Aidha, amewahimiza wahitimu kutumia elimu waliyoipata kama chachu ya mabadiliko chanya katika jamii zao, kwa kuanzisha miradi, kubuni suluhisho za changamoto za kijamii, na kuwa viongozi wenye maono.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili mema, uwajibikaji na uzalendo, akieleza kuwa mambo hayo ni msingi muhimu katika kujenga taifa imara na kuimarisha maendeleo ya Afrika kwa ujumla.
Hotuba yake imepokelewa kwa hisia chanya, ikichukuliwa kama ujumbe wa matumaini kwa kizazi cha vijana na wanawake wanaojitahidi kufikia mafanikio katika mazingira yenye changamoto mbalimbali.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...