Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 11 Aprili, 2026 akiwa Ikulu, Dodoma, amezungumza kwa njia ya mtandao na Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa, Keffi nchini Nigeria, kufuatia kutunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya Bara la Afrika.

Katika hotuba yake, Rais Samia alieleza mshangao wake alipopokea taarifa ya tuzo hiyo kupitia barua kutoka kwa Mheshimiwa Abdullah Isule, Gavana wa Jimbo la Nasarawa. Alisema kilichomgusa zaidi ni kutambuliwa kwa mchango wake katika maendeleo ya Afrika, akibainisha kuwa anapokea heshima hiyo kwa unyenyekevu mkubwa na shukrani.

Amesisitiza kuwa tuzo hiyo si yake binafsi, bali ni ishara ya juhudi za pamoja za Watanzania na matarajio yao ya maendeleo, ushirikiano na ustawi wa binadamu.

Akielezea historia yake, Rais Samia alisema ametoka katika familia ya kawaida na kulelewa katika mazingira ya kijijini yaliyojengwa katika misingi ya unyenyekevu, bidii na maadili ya kijamii. Aliongeza kuwa elimu yake ya awali Zanzibar ilimfungulia macho kuhusu changamoto zinazowakabili wasichana wengi, ikiwemo ukosefu wa rasilimali na mitazamo hasi ya kijamii inayowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

Amesema uzoefu huo ulimjengea azma ya kupambana na vikwazo hivyo si kwa manufaa yake binafsi pekee, bali kwa ajili ya wanawake na wasichana wengine.

Katika safari yake ya uongozi na utumishi wa umma, Rais Samia amejikita katika kuwawezesha wanawake na wasichana kwa kuhamasisha ushiriki wao katika uongozi, elimu na shughuli za kiuchumi. Alisisitiza kuwa hakuna jamii inayoweza kufikia maendeleo ya kweli ikiwa itawaacha nyuma wanawake, ambao ni sehemu kubwa ya jamii.

Aidha, Rais Samia amesema kuwa juhudi zake katika ustawi wa wanawake na watoto zimechangia kuteuliwa kwake na Umoja wa Afrika kuwa kinara wa afya ya mama na mtoto. Pia amewahi kuwa kinara wa biashara huru ya Afrika kwa wanawake na vijana, pamoja na kinara wa nishati safi ya kupikia barani Afrika.

Hotuba yake ilihitimishwa kwa kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na ushirikiano miongoni mwa mataifa ya Afrika ili kufanikisha maendeleo endelevu na ustawi wa watu wake.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...