Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha miundombinu ya elimu nchini inakuwa rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalum, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza elimu jumuishi.

Amesema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo, kufuatia swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum (Wenye Ulemavu), Nasria Nassir Ally, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali katika kuimarisha madarasa pamoja na miundombinu jumuishi katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini.

Akijibu swali hilo, Dkt. Mwigulu alieleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha shule ambazo bado hazijakidhi mahitaji ya miundombinu rafiki, ikiwa ni pamoja na kujenga na kukarabati madarasa, vyoo, pamoja na njia za kupita zinazozingatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.

Alifafanua kuwa katika utekelezaji wa miradi mipya ya ujenzi wa shule, Serikali imeweka kipaumbele kuhakikisha kuwa miundombinu yote inazingatia viwango vya elimu jumuishi, ili kutoa fursa sawa kwa watoto wote kupata elimu bora bila ubaguzi.

“Serikali inahakikisha kuwa shule zote mpya zinazojengwa zinakuwa na mazingira rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalum, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika upatikanaji wa elimu,” alisisitiza Dkt. Nchemba.

Aidha, alibainisha kuwa kwa sasa idadi kubwa ya shule nchini tayari zimeanza kuzingatia mahitaji maalum ya wanafunzi hao, hatua ambayo imechangia kuongeza ushiriki wao katika mfumo rasmi wa elimu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kujenga shule maalum zinazolenga kuhudumia watoto wenye mahitaji maalum, sambamba na kuimarisha miundombinu katika shule za kawaida ili ziweze kuwahudumia wanafunzi wa makundi yote.

Pia alieleza kuwa juhudi zinafanyika katika kuimarisha uwezo wa walimu kwa kuwapatia mafunzo maalum yatakayowawezesha kufundisha wanafunzi wenye mahitaji tofauti kwa ufanisi zaidi. Mafunzo hayo yanahusisha mbinu za ufundishaji jumuishi pamoja na matumizi ya vifaa saidizi vinavyorahisisha ujifunzaji.

Serikali pia imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, wakiwemo mashirika ya ndani na ya kimataifa, katika kuhakikisha kuwa mazingira ya kujifunzia yanaboreshwa na kuwa rafiki kwa kila mwanafunzi bila kujali changamoto alizonazo.

Hatua hizi zinatajwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu jumuishi inayolenga kuhakikisha haki ya elimu inapatikana kwa watoto wote nchini, hususan wale wenye mahitaji maalum.



Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...