-Awapongeza Rais Samia, Rais Mwinyi kwa kuendeleza mafanikio
Na Mwandishi Wetu, Zanziba
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema kazi iliyofanywa na Muasisi wa mapinduzi na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Sheikh Abeid Amani Karume, ndiyo inayowafanya Wazanzibari watembee kifua mbele kwa haki, uhuru na maendeleo.
Aidha, amewapongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Meenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendeleza malengo ya mapinduzi na kuongoza nchi kwa haki.
Wasira aliyasema hayo hivi karibuni, Mjini Unguja katika kongamano la nane la kumuenzi Hayati Karume lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
"Madhumuni ya mapinduzi ya watu wa Zanzibar ni kukomesha upendeleo wa kiuchumi, kijamii na upendeleo wa kisheria, maana uchumi haukuwa kwa Wazanzibari wote, ardhi ilikuwa imechukuliwa na wachache na Wazanzibari watu wazima kazi yao ilikuwa kuangua nazi (wakwezi) kwa wakubwa.
"Mapinduzi yakaleta mabadiliko ambayo yaligawa ardhi ya Zanzibar heka tatu tatu, haki ya uchumi, upendeleo wa sheria kwa maana ya kwamba katika sheria haki unaipata kutegemeana na wewe unatoka wapi hiyo ndio ilikuwa Zanzibar," alisema.
Alisisitiza kumkumbuka hayati Karume, sio kukumbuka miaka yake tangu alipouawa bali ni kukumbuka mazuri aliyoyatenda wakati wa uongozi wake.
"Tunapomkumbuka Karume leo, tunakumbuka mafanikio makubwa ya kuleta umoja wa watu wa Zanzibar. Hivi sasa Zanzibar watu hawabaguliwi kwa misingi hiyo, kazi aliyoianza inaendelea.
"Kwa msingi huo ningependa kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendeleza mawazo hayo ya maendeleo kwa wote," alisema.
HALI ILIVYOKUWA ZANZIBAR
Wasira alisema kongamano hilo shabaha yake ni kutoa elimu kurithisha mambo ya viongozi waliotangulia kwa kizazi kipya.
"Kama hatusemi na wengine wamezaliwa miaka mingi baadae na hawakuwepo wakati wa mapinduzi wanaweza kudhani hivyo walivyo ndivyo walivyokuwa, lakini ukweli ni kwamba Zanzibar kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine katika Afrika hata Zanzibar haki ilikuwa kitu adimu sana kukipata kwa sababu haki ilitolewa kulingana na mahitaji ya rangi ya watu kabila zao, asili yao," alieleza
Kwa mujibu wa Wasira, wakati wa utawala wa Sultan kama mwananchi hakuwa na asili iliyompendeza mtawala hakupewa haki.
"Kama asili yako haikumpendeza (Sultan) unanyimwa haki, hivyo ndivyo ilivyokuwa. Tunapomkumbuka Hayati Abeid Amani Karume vijana lazima wajue hatukumbuki miaka 54 ya kuuawa kwake, tunakumbuka mchango wake na fikra zake zilizoifikisha Tanzania hapa ilipo, hicho ndicho tunachokumbuka.
Ukikumbuka miaka 54 ya kifo chake hujakumbuka kitu maana hata Afro Shirazi wakati alipouawa walisema wameua kiwiliwili lakini mawazo yamebaki, kwa kauli ya Afro Shirazi mwaka 1972 kilichoondoka ni kiwiliwili cha Karume lakini mawazo yake yanaendelea. Kwa maneno mengine hawakuua mapinduzi waliua mtu.
"Hivyo ndivyo ilivyokuwa Zanzibar kupata haki ni mpaka ujulikane wewe hasa unatokana na kundi lipi...jitihada kubwa za serikali ya Sultan na washirika wake Waingereza ilikuwa kugawa watu, unawagawa halafu unawatawala, unawachonganisha. Hivi ndivyo ilivyokuwa.
"Chama cha Afro Shirazi kitu ambacho walikuwa wanapinga ni kupindisha haki, walikuwa wanataka haki ziende kwa wote bila kujali dini, bila kujali makundi, bila kujali asili ya mtu anakotokea. Hiyo ndio ilikuwa kazi ya Afro Shirazi na ninao ushahidi wa jambo hilo.
Februari 25, 1964 kwa sababu hapakuwa na Bunge hapa, kulikuwa na Baraza la Mapinduzi ndilo lilikuwa linatunga sheria na ndilo lilikuwa linampa mamlaka rais atunge sheria zinazoambatana na sera na Ilani ya Chama cha Afro Shirazi, kwa hiyo tarehe ile Rais alitunga sheria inaitwa DP, na dp ile ilikuwa inasema sheria itakuwa inajulikana kwa jina la usawa, maridhiano na umoja wa watu wa Zanzibar, hiyo ilikuwa mwaka 1964 mwezi mmoja baada ya mapinduzi," alisema.
Wasira alisema Mapinduzi yalileta mabadiliko ambayo yaligawa ardhi ya Zanzibar heka tatu tatu kwa mwananchi.




.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...