Na Asia Singano na Josephine Majura, WF, Mwanza.
SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia sera na mipango mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), katika Mahafali ya 20 ya Shule ya Sekondari ya Thaqaafa, wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Alieleza kuwa, Serikari inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia Sera na mipango mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ili kuhakikisha kuwa vijana wanapata fursa za kuendeleza vipaji vyao na kuchangia kikamilifu maendeleo ya taifa.
‘’Dunia ya sasa inahitaji vijana wanaoweza kutatua changamoto kwa ubunifu, hasa katika nyanja za uchumi, teknolojia na ujasiriamali ‘’ Alisema Mhe. Munde (Mb).
Amewaasa vijana kuendelea kuwa na nidhamu na uadilifu kwakuwa Taifa linahitaji vijana wenye misingi imara ya maadili, wanaoweza kusimamia rasilimali za nchi kwa uwajibikaji na weledi.
Kwa upande wake Meneja wa Shule ya Thaqaafa, Bw. Idrisa Hayeshi, amewasisitiza wazazi kuendelea kushirikiana na walimu na Uongozi wa shule kufuatilia maendeleo ya wanafunzi ili kujua mwenendo wa tabia ambazo zina athari katika masomo yao.
“Shule imejipanga kutoa elimu bora ikiwa na matokeo mazuri kwa kila mwaka, tunavyofanya mawasiliano na mzazi ni kwamba atoe ushirikiano ili mtoto apate kitu kinachostahili’’ alisema Bw. Hayeshi.
Shule ya Sekondari Thaqaafa imeadhimisha Mahafali ya 20 ya Kidato cha Sita ambayo yalihudhuriwa na wahitimu (50).



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...