Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha mapinduzi ya kidigitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia uwekezaji mkubwa katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kupunguza urasimu katika taasisi za umma.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali imechukua hatua za makusudi kuhakikisha huduma zinapatikana kwa haraka na kwa njia rahisi zaidi kupitia mifumo ya kidigitali.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya mifumo 252 ya serikali imeunganishwa katika mtandao mmoja wa kidigitali unaowezesha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za umma.

Kwa mujibu wa Ridhiwani, hatua hiyo imeiwezesha serikali kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi bila ulazima wa kufika ofisini, jambo ambalo limepunguza msongamano na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi za umma.

Aidha, amesema mabadiliko hayo yameleta nafuu kubwa kwa wananchi kwa kupunguza muda na gharama walizokuwa wakitumia kufuata huduma mbalimbali za serikali, ambazo sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao.

Waziri huyo amesema kuwa maboresho hayo pia yamechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza urasimu uliokuwa ukikwamisha upatikanaji wa huduma, hususan katika taasisi ambazo zilitegemea zaidi mifumo ya karatasi.

Ameongeza kuwa kuunganishwa kwa mifumo hiyo ya TEHAMA kumeongeza uwazi katika utendaji wa kazi za serikali, kwani taarifa sasa zinapatikana kwa urahisi na zinaweza kufuatiliwa kwa wakati halisi.

Ridhiwani amesema uwazi huo umeimarisha pia uwajibikaji ndani ya taasisi za umma, kwani kila hatua ya utoaji huduma inaweza kufuatiliwa na kudhibitiwa kupitia mifumo ya kidigitali.

Aidha, amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA na kuboresha mifumo iliyopo ili kuhakikisha huduma za umma zinakuwa za kisasa zaidi na zinakidhi mahitaji ya wananchi.

Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha Tanzania inakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani, huku ikiboresha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kupitia mifumo ya kidigitali yenye ufanisi mkubwa.

Serikali imeeleza kuwa mageuzi hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha utawala bora na kuongeza tija katika sekta ya umma, ikiwa ni pamoja na kupunguza mianya ya upotevu wa rasilimali na kuongeza uwajibikaji.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...