Maofisa wawili wa wakala wa misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Makete mkoani Njombe wamehukumiwa Kifungo cha miaka miwili jela ama kulipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja baada ya kukutwa na hatia ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni 8 kwa Yuda Male mkazi wa kijiji cha Mfumbi kata ya Mfumbi wilayani hapo ambaye ni mfugaji baada ya kuingiza mifugo katika Msitu wa asili wa serikali wa Chimala.
Akitoa hukumu katika mahakama ya wilaya ya Makete Aprili 16, 2026 Hakimu mkazi Mfawidhi Mwandamizi mahakama hiyo Irvan Msacky amesema mshitakiwa Thadeus James Mtui(31) mhifadhi TFS Matamba na Florian Giliad Kilango(33) afisa wa TFS wilaya ya Makete
kwa nyakati tofauti watumishi hao walichukua rushwa kwa mfugaji huyo baada ya kumkuta akilisha mifugo katika Msitu wa asili wa serikali kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 marejeo ya Mwaka 2024.
Katika mashtaka hayo ambayo yalifunguliwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Makete, Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU mkoa wa Njombe Daniel Mono ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho hasa ukizingatia mkakati wa serikali ni kutunza na kulinda mazingira na maliasili zake
Watuhumiwa hao wamekiri kutenda makosa hayo ya kuomba na kupokea rushwa na ndipo wakahukumiwa na mahakama hiyo, lakini ili kukwepa kifungo cha miaka miwili jela wakalipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja.
Washitakiwa Thadeus James Mtui na Florian Gilliad Kilango walichukua rushwa ya kwanza mnamo tar 1/11/2025 kiasi cha Milioni 2 baada ya kukamata mifugo ya Yuda Male na kisha kuchukua rushwa nyingine kiasi cha milioni 6 mnamo 31/1/2026 baada ya kushika tena mifugo ya mfugaji huyo katika Msitu uleule wa asili wa Chimala uliopo kijiji cha Mfumbi kata ya Mfumbi wilayani hapo.
Licha kukiri kosa lao na kisha kulipa faini, Mahakama hiyo imeagiza wawili hao pia kurejesha fedha yote waliyochukua kwa mfugaji huyo kiasi cha shilingi milioni 8 ambaye inaelezwa aliamua kuripoti katika vyombo vya dola kutokana usumbufu alioendelea kuupata ili hali aliwapa rushwa watumishi hao.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...