Na Mwandishi Wetu-DODOMA

Serikali imesisitiza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatoa kipaumbele cha pekee kwa ushiriki wa vijana katika maendeleo, kwa lengo la kuinua vipaji, uwezo, na ari yao katika kufanikisha ukuaji wa uchumi jumuishi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi,  leo tarehe 29 Aprili, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la kwanza la kisayansi la vijana kuhusu VVU/UKIMWI, afya ya uzazi, jinsia na masuala mtambuka. Kongamano hilo limeandaliwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Kabudi alisisitiza kuwa dhamira kuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kujenga taifa lenye nguvukazi iliyoelimika, yenye ujuzi na maono.

"Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatoa kipaumbele kwa vijana kwa kutumia vipaji na uwezo wao katika kufanikisha maendeleo endelevu. Nguvukazi hii itajengwa katika misingi imara ya ubunifu, ujasiriamali, na uwajibikaji," amesema Prof. Kabudi.

Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele katika kushughulikia changamoto za ukatili wa kijinsia na afya ya akili.

Ameeleza kuwa, serikali imeanzisha madawati maalum ya ulinzi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo shuleni, vyuoni, na kwenye ngazi ya jamii ili kuhakikisha huduma za kinga na msaada zinawafikia wahitaji kwa wakati.

Awali, akimkaribisha Waziri, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. James Kilabuko, amebainisha umuhimu wa kongamano hilo kwa ustawi wa vijana.

"Kongamano hili ni chachu ya mabadiliko ya fikra na utendaji, tunatarajia elimu watakayopata itakuwa mwanzo wa safari ya kujenga jamii yenye afya, matumaini, na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wao," amesema  Dkt. Kilabuko.

Kongamano hilo la siku mbili linaongozwa na kaulimbiu; ‘’Kuunganisha Sayansi na Ubunifu katika Kukabiliana na Janga la VVU, Afya ya Uzazi na Jinsia, Kukuza Ustawi Kuelekea Dira 2050”.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...