Na Mwandishi Wetu, Kaliua – Tabora


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti, umeshiriki uzinduzi wa Maonesho ya Jukwaa la Tatu la Maendeleo ya Ushirika yanayofanyika wilayani Kaliua, mkoani Tabora, huku ukitumia jukwaa hilo kuhamasisha uhifadhi wa misitu na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

Maonesho hayo yamezinduliwa Aprili 29, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa leo Aprili 30, 2026, yakibeba kaulimbiu isemayo “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”, ikiwa ni wito kwa wadau kuimarisha misingi ya uwajibikaji na usimamizi bora wa vyama vya ushirika.

Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Kituo cha Uzalishaji Mbegu za Miti, Mhifadhi Medard Nogorya alieleza kuwa ushiriki wa TFS unalenga kusogeza huduma kwa wananchi pamoja na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa upandaji miti na uhifadhi wa misitu katika kukuza uchumi wa jamii.

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mheshimiwa Gerald Mongella, alipata fursa ya kutembelea banda la TFS na kupatiwa maelezo kuhusu shughuli za uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za miti, pamoja na mchango wake katika kuimarisha sekta ya misitu nchini.

Sambamba na maonesho hayo, TFS ilitumia pia vyombo vya habari kuifikia jamii kwa upana zaidi, ambapo ilitoa elimu ya uhifadhi kupitia kituo cha redio cha CG FM kinachosikika mkoani Tabora na wilaya zake, hatua inayolenga kuongeza mwamko wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za misitu.

Ushiriki wa TFS katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha uhusiano na wadau, kukuza uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi, na kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali za misitu kwa maendeleo endelevu.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...