JESHI la Polisi Mkoa wa Rukwa linaendelea na mapambano dhidi ya wahalifu mbalimbali wakiwemo wale wanaosababisha taharuki katika jamii kwa kuzusha kuibiwa sehemu nyeti za miili yao na wale wanaowafanyia ukatili na udhalilishaji watoto.

Katika kuhakikisha jamii ya watu wa Mkoa wa Rukwa wanaishi bila hofu, limewafikisha mahakamani tena vijana watatu waliomzushia bwana Hosea Ngogo (31) mkazi wa Soweto Mbeya kuwaibia nyeti zao katika kijiji cha Kilangawana wilaya ya Sumbawanga kisha kumpiga na kumsababishia jeraha kichwani.

Vijana hao ambao ni Geofrey Milumba Deminic (24), Jafari Nebart Shanjila (25) wakazi wa Kijiji cha Kilangawana pamoja na Huruma Geofrey Kasonso (18) mkazi wa Kijiji cha Kilyamatundu, wametiwa hatiani na mahakama ya mwanzo Kipeta mbele ya Mhe. Hakimu Wilgis Mbunda.

Wote watatu wamepewa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela kila mmoja, pia kumlipa fidia ya maumivu na jeraha alilopata bwana Hosea Amani Ngogo kiasi cha Tsh.50,000/= kila mmoja. Adhabu hiyo imetolewa 10 April, 2026 na hakimu huyo huku akisema iwe funzo kwa wote wanaozusha mambo ya kishirikina na kuleta hofu katika jamii ya watanzania waliostaarabika.

Kwa upande mwingine, mahakama ya wilaya ya Nkasi tarehe 09 Aprili 2026, imemhukumu Wandu Frolian Chimukole (30) mkazi wa kijiji cha Mbwendi wilayani Nkasi kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatika na hatia ya kumbaka binti mwenye umri wa miaka 13. Mshitakiwa huyu alitenda kosa hilo tarehe 20 Januari 2026 huko kijiji cha Kakoma Wilaya ya Nkasi. Wakati akitoa adhabu hiyo Mhe. Hakimu Denis Luwungo alisema adhabu hiyo iwe onyo kwa wanaume wenye tabia ya kuwafanyia ukatili watoto wadogo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutii sheria za nchi, pia wazazi kuendeleza ulinzi wa watoto ili wasifanyiwe ukatili.

Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,

Mkoa wa Rukwa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...