Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Samson Allute.
Mwezeshaji Mafunzo, Osiah Mwanyesya.

Na Mwandishi Wetu
WALIMU wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati nchini, wametakiwa kutumia teknolojia pamoja na mbinu bunifu za ufundishaji ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi na kusaidia kuzalisha wataalamu wa sayansi watakaochangia maendeleo ya taifa kijamii na kiuchumi.

Wito huo umetolewa Aprili 29, 2026 na Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Samson Allute, wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa walimu wa Sayansi na Hisabati kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu.

Allute amesema matumizi ya teknolojia katika ufundishaji yatawawezesha walimu kufundisha kwa ufanisi zaidi huku yakichochea wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi na Hisabati tangu wakiwa mashuleni.

Amesema serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP), unaolenga kuboresha miundombinu ya shule, kutoa mafunzo kazini kwa walimu pamoja na kuimarisha matumizi ya vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Mwalimu anapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri, kufanya ubunifu na kuwa wataalamu watakaosaidia maendeleo ya taifa,” amesema Allute.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia teknolojia na mbinu shirikishi za ufundishaji ili kuboresha ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya Sayansi na Hisabati.

Aidha, amewataka walimu kutumia maarifa watakayoyapata kuwasaidia wanafunzi kuondoa hofu ya masomo ya sayansi ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakionekana kuwa magumu kwa baadhi yao.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Happiness Goyi, mwalimu wa Kemia kutoka Shule ya Sekondari Mwakibuga mkoani Simiyu, amesema mafunzo hayo yatamsaidia kutumia mbinu za kisasa zitakazowawezesha wanafunzi kuelewa kwa urahisi masomo ya sayansi na kuyapenda zaidi.

Naye Daniel David, mwalimu wa Fizikia, amesema matumizi ya teknolojia katika ufundishaji yatawasaidia wanafunzi kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa sayansi na teknolojia.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo walimu 523 kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora na Katavi kupitia mradi wa SEQUIP.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...