Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya afya baada ya kiwango cha utoaji wa chanjo nchini kufikia asilimia 96, hatua inayotajwa kuwa ni mafanikio makubwa katika kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa kwa watoto na wananchi kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa (MB), wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni, ambapo amesema ongezeko hilo limetokana na juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za msingi za afya pamoja na kuongeza upatikanaji wa chanjo katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kiwango hicho kimeongezeka kutoka asilimia 93 hadi asilimia 96, jambo linaloifanya Tanzania kuvuka lengo la kimataifa la asilimia 90 lililowekwa kwa ajili ya utoaji wa chanjo.
“Kuongezeka kwa kiwango hiki ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya afya, hususan kwenye huduma za kinga na chanjo ambazo zimeendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini,” amesema Mchengerwa.
Aidha, Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa chanjo kwa kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa urahisi katika vituo vya afya, zahanati na hospitali nchini kote ili kuongeza ulinzi dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha afya ya mama na mtoto pamoja na kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza ambayo yanaweza kuzuilika kupitia chanjo.
Mbali na hilo, Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata chanjo pamoja na kushiriki katika kampeni mbalimbali za afya zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kinga na huduma za afya za msingi.
Wadau wa afya wameendelea kuipongeza Serikali kwa hatua hiyo wakieleza kuwa kuongezeka kwa kiwango cha chanjo kutasaidia kujenga jamii yenye afya bora na kupunguza mzigo wa magonjwa nchini.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, utoaji wa chanjo kwa kiwango kikubwa ni moja ya njia muhimu za kudhibiti magonjwa hatari kwa watoto na jamii kwa ujumla, huku mafanikio hayo yakitajwa kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuendelea kuboresha sekta ya afya na huduma za kinga.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...