Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
FAMILIA bora imeelezwa kuwa msingi muhimu wa kujenga taifa lenye maadili, nidhamu na upendo, huku wazazi na walezi wakitakiwa kuzingatia malezi yenye usawa wa kijinsia na mawasiliano mazuri ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye ustawi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Malezi na Familia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Carlos Gwamagobe, wakati akitoa mafunzo katika mafunzo maalum kwa waandishi wa habari za watoto kutoka mikoa mbalimbali nchini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Gwamagobe alisema serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yanayozingatia upendo, ulinzi, maadili na usawa wa kijinsia kwa kuwa watoto wa leo ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa la kesho.

Alisema wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao kwa kuwasikiliza, kuwapa muda na kuwalea katika mazingira yasiyo na ukatili ili kuwajengea kujiamini na kukuza ustawi wao.

“Familia bora hujenga watoto wenye maadili mema ambao baadaye huwa wananchi wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Gwamagobe.

Aidha, alisema ushirikiano kati ya serikali, vyombo vya habari na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhamasisha malezi bora yatakayosaidia kujenga familia imara na watoto wenye maadili mema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya Malezi na Familia kutoka wizara hiyo, Victor Rugarabamu, alisema tafiti zinaonyesha kuwa kukosekana kwa malezi yanayozingatia usawa wa kijinsia ni miongoni mwa sababu zinazochangia kudorora kwa ustawi wa watoto nchini.

Alisema kupitia mafunzo hayo, wizara inatarajia kuona vipindi vinavyorushwa kupitia redio za jamii, televisheni na mitandao ya kijamii vikitoa elimu ya maadili mema, kuhamasisha malezi bora na kuwasaidia watoto pamoja na vijana balehe kukua katika mazingira salama yenye upendo na ulinzi.

“Waandishi wa habari mna nafasi kubwa ya kuelimisha jamii kupitia maudhui wanayoandaa. Tunahitaji vipindi vinavyofundisha, kuburudisha na kujenga maadili kwa watoto,” alisema Rugarabamu.

Naye Mkufunzi wa Malezi ngazi ya Taifa, Sabrina Majikata kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la ICS, alisema mafunzo hayo yamejikita katika nguzo kuu tatu za malezi ambazo ni kumjali mtoto, kumlinda na kuzungumza naye kwa karibu.

Alisema wazazi wengi wanakosa muda wa kukaa na watoto wao hali inayochangia kupungua kwa mawasiliano ndani ya familia na kusababisha watoto kukosa nafasi ya kueleza changamoto wanazokutana nazo.

“Mwandishi wa habari anapokuwa na uelewa kuhusu ukuaji wa watoto na changamoto zinazowakabili, anakuwa na uwezo mkubwa wa kuandaa maudhui yenye manufaa kwa jamii,” alisema Sabrina.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabia za Jamii kutoka UNICEF, Alice Mwiru, alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha ustawi wa watoto na kuhakikisha haki zao zinapewa kipaumbele kupitia vyombo vya habari.

Alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kutumia ubunifu, lugha rafiki kwa watoto na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari katika kuandaa vipindi vinavyochangia ukuaji na maendeleo ya mtoto.

Washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kuandaa maudhui yanayowagusa watoto na vijana kwa njia sahihi na yenye kujenga jamii yenye maadili mema.

“Mafunzo haya yamenipa uelewa mpana kuhusu namna ya kuandaa maudhui yanayofundisha na kuburudisha kwa wakati mmoja huku yakizingatia hatua za ukuaji wa mtoto,” alisema Mika Ndaba




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...