Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon zitakazofanyika Julai 26, 2026 jijini Dodoma, huku waandaaji wakijiwekea lengo la kuvunja rekodi mpya ya ushiriki kwa kuvutia wakimbiaji zaidi ya 15,000 kutoka ndani na nje ya nchi.

Baada ya kuvutia washiriki zaidi ya 12,000 msimu uliopita, mbio hizo sasa zinaendelea kujijengea hadhi ya kuwa miongoni mwa marathon kubwa na zenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Tanzania, si tu kwa upande wa michezo bali pia katika kuchochea agenda za kijamii na afya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema msimu huu wa saba unakuja ukiwa na dhamira mpya ya kugusa maisha ya Watanzania wengi zaidi kupitia nguvu ya michezo.

“Tunapoendelea kuikuza NBC Dodoma Marathon, tunataka kuona mbio hizi zikibaki kuwa zaidi ya mashindano ya riadha. Hii ni mbio ya matumaini, mbio ya afya na mbio ya kuokoa maisha,” alisema Sabi.

Kwa mujibu wa Sabi, msimu huu wa NBC Dodoma Marathon unalenga kukusanya fedha zitakazosaidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua, kusaidia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na kuimarisha mfuko wa huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye changamoto ya selimundu (sickle cell).

Uzinduzi huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa mbio hizo wakiwemo viongozi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Benjamin Mkapa, Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) ambazo ni wanufaika wa mbio hizo, wadhamini pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.

Katika msimu huu, kama ilivyo kawaida, washiriki watashiriki katika mbio za kilomita 5, kilomita 10, Nusu Marathon (KM 21) pamoja na Marathon Kamili ya kilomita 42 inayotarajiwa kuvuta ushindani mkali wa wakimbiaji wa ndani na wa kimataifa.

Sabi alisema katika kipindi cha miaka sita tangu kuanzishwa kwa NBC Dodoma Marathon, mbio hizo zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zilizosaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya nchini.

Alisema zaidi ya asilimia 80 ya fedha hizo zimeelekezwa katika mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kupitia ushirikiano na Taasisi ya Saratni ya Ocean Road, ambapo zaidi ya wanawake 200,000 wamefanyiwa uchunguzi wa afya na wengine kupata matibabu yaliyosaidia kupona kabisa.

“Aidha, tangu mwaka 2023 tumefanikiwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 400 zilizowezesha ufadhili wa masomo ya diploma kwa wakunga 200 kupitia ushirikiano wetu na Taasisi ya Benjamin Mkapa. Lengo ni kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi, na mwaka huu tunatarajia kuongeza wigo kwa kuwafikia wakunga wengi zaidi,” alisema.

Kwa mujibu wa Sabi, NBC kupitia msimu huu pia imetenga shilingi milioni 200 kusaidia upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na JKCI pamoja na kiasi kingine cha shilingi milioni 200 kitakachosaidia huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye selimundu kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa.

“Haya yote yanawezekana kutokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wetu ambao wameendelea kusimama nasi tangu mwanzo wa safari hii. Tunawashukuru sana wadhamini wetu wote na wadau wengine wengi kwa kuwa pamoja kwenye jitihada hizi muhimu,” aliongeza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo kwa sasa ina zaidi ya watoto 1,500 wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo, huku gharama za matibabu hayo zikifikia kati ya shilingi milioni 4 hadi 8 kwa kila mtoto.

“NBC Dodoma Marathon imeongeza matumaini kwa familia nyingi zenye watoto wenye changamoto za moyo. Mchango huu utasaidia ununuzi wa vifaa tiba na kuongeza uwezo wa utoaji huduma za matibabu. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watoto 100 wanaozaliwa, wawili huzaliwa na matatizo ya moyo,” alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa mbali na kusaidia matibabu, mbio hizo zimekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha jamii kuhusu mazoezi na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi alisema gharama za huduma za upandikizaji wa uloto kwa mtoto mmoja mwenye selimundu zinaweza kufikia shilingi milioni 200, hivyo ushirikiano huo utasaidia kuongeza uwezo wa mafunzo kwa wataalamu wa tiba hiyo nchini.

“Hadi sasa watoto 30 tayari wamefanyiwa upandikizaji wa uloto na wamepona. Malengo yetu ni kuongeza idadi hiyo hadi watoto 30 kila mwaka kutoka kiwango cha sasa cha watoto 10. Tunaamini NBC Dodoma Marathon itaendelea kuwa kichocheo kikubwa cha matumaini kwa watoto hawa na familia zao,” alisema Prof. Makubi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benjamin Mkapa Foundation, Dkt. Ellen Mkondya-Senkoro alisema ushirikiano wao na NBC Dodoma Marathon tangu mwaka 2023 umewezesha kutoa mafunzo kwa wakunga na wauguzi 200 kutoka hospitali mbalimbali za umma ambao sasa wanatoa huduma katika vituo vya afya zaidi ya 150 vilivyopo kwenye wilaya 31 nchini.

Wakizungumza kwa niaba ya wadhamini wa mbio hizo, viongozi kutoka Sanlam Allianz Tanzania na GSM Group walisema wameendelea kuunga mkono NBC Dodoma Marathon kutokana na dhamira yake ya kutumia michezo kama jukwaa la kuokoa maisha na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Usajili wa mbio za NBC Dodoma Marathon umefunguliwa rasmi hatua inayotoa fursa kwa washiriki kuweza kujisajili kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz na kuchangia kiasi cha TZS 45,000 kwa usajili wa mtu mmoja mmoja au 42,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu 30 au zaidi.




Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kushoto), akiongoza mbio za majaribio sambamba na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dkt Ellen Mkondya-Senkoro (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benjamin Mkapa Hospital, Prof Abel Makubi (kulia), pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt Peter Kisenge (wa pili kulia), wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zitafanyika Julai 26, 2026 jijini Dodoma na zinatarajiwa kuvutia zaidi ya wakimbiaji 15,000, huku zikilenga kuchangisha fedha za kusaidia mapambano dhidi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi, upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye changamoto ya selimundu (sickle cell).






Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (pichani), akiongoza zoezi la uzinduzi rasmi wa msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zitafanyika Julai 26, 2026 jijini Dodoma na zinatarajiwa kuvutia zaidi ya wakimbiaji 15,000, huku zikilenga kuchangisha fedha za kusaidia mapambano dhidi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi, upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye changamoto ya selimundu (sickle cell).





Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio za NBC Dodoma Marathon, Bi Tatiana Masimba (pichani) akizungumza kwenye hafla hiyo.






Wakizungumza kwa niaba ya wadhamini wa mbio hizo, viongozi kutoka Sanlam Allianz Tanzania na GSM Group walisema wameendelea kuunga mkono NBC Dodoma Marathon kutokana na dhamira yake ya kutumia michezo kama jukwaa la kuokoa maisha na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.






Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema msimu huu wa saba unakuja ukiwa na dhamira mpya ya kugusa maisha ya Watanzania wengi zaidi kupitia nguvu ya michezo.






Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, sambamba na wadau wengine wakifanya mbio za majaribio wakati wa uzinduzi rasmi wa msimu wa saba wa mbio za kimataifa za NBC Dodoma Marathon uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zitafanyika Julai 26, 2026 jijini Dodoma na zinatarajiwa kuvutia zaidi ya wakimbiaji 15,000, huku zikilenga kuchangisha fedha za kusaidia mapambano dhidi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa uzazi, upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na huduma za upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye changamoto ya selimundu (sickle cell).















Uzinduzi huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa mbio hizo wakiwemo viongozi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Benjamin Mkapa, Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) ambazo ni wanufaika wa mbio hizo, wadhamini pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...