Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imezindua rasmi mfuko maalumu wa kuchangia huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, ukiwa na lengo la kuimarisha upatikanaji wa matibabu ya upandikizaji viungo nchini, huku mafanikio makubwa yakiripotiwa kwa watoto 30 waliopandikizwa uloto na kupona.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, amesema uanzishwaji wa mfuko huo umetokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za upandikizaji viungo pamoja na uhitaji wa kushirikisha wadau mbalimbali katika kuunga mkono jitihada za serikali.

Profesa Makubi ameeleza kuwa hospitali hiyo imepiga hatua kubwa katika huduma za kibingwa, ambapo upandikizaji wa figo ulianza mwaka 2018 na hadi sasa wagonjwa 56 tayari wamenufaika kwa mafanikio makubwa.

Aidha, amesema huduma ya upandikizaji wa uloto ilianza mwaka 2023 na hadi sasa watoto 30 wamefanyiwa upasuaji huo na wote wanaendelea vizuri kiafya, hatua inayoonesha maendeleo makubwa ya tiba za kibobezi nchini.

Ameongeza kuwa mfuko huo utasaidia si tu wagonjwa wanaosubiri matibabu, bali pia kupanua miundombinu na kuboresha huduma za kibingwa ili kufikia wagonjwa wengi zaidi.

Katika hatua nyingine, Profesa Makubi amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechangia Shilingi bilioni 1 kusaidia huduma hizo, huku akisisitiza umuhimu wa wadau wengine kuendelea kushiriki.

WITO WA USHIRIKIANO KUIMARISHA HUDUMA ZA FIGO NA SIKOSELI

Kwa upande wake, Naibu Spika Daniel Sillo amesema ushiriki wa wananchi, taasisi na wadau binafsi ni muhimu katika kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa sugu ikiwemo figo na sikoseli.

Amesema gharama za matibabu ya kibingwa bado ni kubwa, hivyo haziwezi kubebwa na serikali pekee, jambo linalohitaji mshikamano mpana wa jamii nzima.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni kilichowakutanisha viongozi na wadau wa afya, Sillo amesema michango ya hiari inaweza kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wanaohitaji upandikizaji na matibabu maalumu.

Ameongeza kuwa magonjwa hayo hayabagui mtu kwa nafasi, kipato au hali ya maisha, hivyo ni jukumu la pamoja kuhakikisha kila mwenye uhitaji anapata matibabu kwa wakati.

Sillo amesisitiza kuwa kuongezeka kwa michango kutasaidia pia kuboresha miundombinu ya afya na kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kibingwa ndani ya nchi badala ya wagonjwa kusafirishwa nje kwa gharama kubwa.

Kwa ujumla, jitihada hizo za BMH pamoja na wito wa wadau zinaendelea kuonesha mwelekeo chanya wa Tanzania kupunguza utegemezi wa matibabu ya nje na kuimarisha huduma za kibingwa ndani ya nchi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...