Na Janeth Raphael MichuziTv- Bungeni Dodoma.
Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, amesema kuwa maendeleo makubwa yanayoendelea kufanyika katika Jiji la Dodoma hayapaswi kutafsiriwa kama upendeleo wa Serikali kwa mkoa huo, bali ni utekelezaji wa wajibu wa kitaifa kutokana na hadhi ya Dodoma kuwa makao makuu rasmi ya nchi.
Simbachawene ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika mchango wake, mbunge huyo alisema kumekuwepo na maneno pamoja na minong’ono kutoka kwa baadhi ya watu wakidai kuwa Dodoma inapendelewa kwa kupewa fedha nyingi na miradi mikubwa ya maendeleo ikilinganishwa na maeneo mengine ya Tanzania.
Hata hivyo, Simbachawene amesisitiza kuwa hoja hizo hazina msingi, akieleza kuwa Dodoma ni makao makuu ya Watanzania wote na si mali ya kundi, mkoa au eneo fulani pekee.
“Dodoma ni makao makuu ya nchi. Ni ya Watanzania wote. Hatuwezi kuizungumza Dodoma kana kwamba ni eneo la watu wachache au linafanyiwa upendeleo maalum,” alisema Simbachawene bungeni.
Alifafanua kuwa uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali pamoja na hadhi ya makao makuu ya nchi kwenda Dodoma ulifanywa kwa mujibu wa sheria na maamuzi ya kitaifa yaliyolenga kuijenga Tanzania kwa usawa na ufanisi mkubwa wa kiutawala.
Kwa mujibu wa Simbachawene, sheria hiyo iliyopitishwa miaka ya nyuma ndiyo iliyoweka msingi wa Dodoma kupewa hadhi maalum ya kuwa kitovu cha utawala wa nchi, hivyo ni jambo la kawaida kwa Serikali kuelekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa miundombinu, barabara, taasisi pamoja na huduma mbalimbali muhimu katika jiji hilo.
Amesema nchi nyingi duniani huwekeza kwa kiwango kikubwa katika miji yao ya makao makuu ili kuhakikisha inakuwa mfano wa maendeleo, utawala bora na utoaji wa huduma, hivyo Tanzania nayo haina budi kufanya hivyo kwa Dodoma.
Mbunge huyo ameongeza kuwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan katika kuibadilisha Dodoma itaendelea kukumbukwa katika historia ya taifa.
Alieleza kuwa maendeleo yanayoonekana sasa katika sekta ya miundombinu, hususan barabara na huduma za kijamii, ni sehemu ya safari ya kuifanya Dodoma kuwa jiji la kisasa linaloakisi hadhi ya Tanzania kama taifa.
“Historia itaandika kazi kubwa inayofanyika Dodoma. Hii ni kazi ya kizalendo na ya kutukuka kwa manufaa ya Watanzania wote,” aliongeza.
Simbachawene pia aliwataka Watanzania kuangalia maendeleo ya Dodoma kama uwekezaji wa kitaifa wenye manufaa mapana kwa nchi nzima, badala ya kuyaona kama kipaumbele kinachowanyima haki wananchi wa maeneo mengine.
Amesisitiza kuwa maendeleo ya makao makuu ya nchi yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuboresha utendaji wa Serikali na kuimarisha taswira ya taifa ndani na nje ya Tanzania.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...