Britam Insurance Limited (Tanzania) imewekeza TZS milioni 40 katika mradi wa maji safi unaolenga shule mbili za msingi jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu inayokabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji salama katika taasisi za umma.
Mradi huo, uliotekelezwa kwa ushirikiano na kampuni ya uhandisi ya Davis & Shirtliff, umehusisha ufungaji wa mifumo ya pampu za maji zinazotumia nishati ya sola katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo Ilala na Shule ya Msingi Mshikamano iliyopo Kivule. Kama sehemu ya juhudi za utunzaji wa mazingira, shughuli za upandaji miti pia zilifanyika katika Shule ya Msingi Mshikamano ili kusaidia uhifadhi wa mazingira.
Mtendaji Mkuu wa Britam Tanzania, Farai Dogo, alisema kuwa “mradi huu umebuniwa kushughulikia changamoto za kijamii na kimazingira, huku ukipunguza utegemezi wa umeme katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa uhakika.”
Meneja wa Masoko wa Britam, Leoncia Makubo, alisema mifumo hiyo ilikamilika baada ya kufanyika utafikia wa mahitaji mwezi Mei 2025, iliyochunguza changamoto za upatikanaji wa maji katika shule mbalimbali kabla ya kuchagua shule hizo mbili kunufaika na mradi huo.
“Uwekezaji huu unaakisi mkakati wetu wa kuwezesha jamii kupitia suluhisho endelevu zinazosaidia pia kulinda mazingira,” alisema Dogo wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mifumo ya maji inayotumia nishati ya sola inatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 10,000, wakiwemo wanafunzi, walimu, pamoja na jamii inayozunguka shule hizo kwa kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama.
Katika Shule ya Msingi Mshikamano, mradi huo unatarajiwa kusaidia shughuli za kila siku za shule ikiwemo maandalizi ya chakula kwa wanafunzi wa awali, sambamba na kuboresha hali ya usafi na mazingira ya afya. Zoezi la upandaji miti lililofanyika shuleni hapo pia linaongeza uelewa wa utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi na kusaidia juhudi za uendelevu wa muda mrefu.
Katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, viongozi wa mradi walieleza kuwa mradi huo utasaidia kuimarisha mazingira jumuishi ya elimu, ikiwemo kuboresha mazingira kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Dogo aliongeza kuwa “matumizi ya teknolojia ya pampu za maji zinazotumia nishati ya sola yatasaidia kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa pamoja na gharama za uendeshaji ukilinganisha na mifumo inayotumia dizeli au umeme wa gridi, jambo linaloendana na malengo mapana ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.”
Mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa uwajibikaji kwa jamii wa Britam. Kati ya mwaka 2024 na 2025, Britam imesaidia zaidi ya shule 70 kupata huduma bora za maji, imechangia upandaji wa zaidi ya miti 95,000, na kuwafikia zaidi ya watu 90,000 Afrika Mashariki kupitia miradi ya maji, elimu na mazingira.
Kampuni hiyo pia inalenga kupanda miti milioni 6 nchini Tanzania ifikapo mwaka 2030 kama sehemu ya lengo la Britam Group la kupanda miti milioni 60 katika ukanda wa Afrika Mashariki na nchi nyingine ambako kampuni hiyo inaendesha shughuli zake.
Davis & Shirtliff, waliotoa na kufunga mifumo hiyo ya pampu za maji, walisema mifumo hiyo imeundwa kwa ubora wa kudumu kwa muda mrefu na kuhitaji matengenezo madogo, hasa katika maeneo yasiyo na umeme wa uhakika.


.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...