Na MWANDISHI WETU
DIWANI wa Kata ya kisutu, jijini Dar es Salaam, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM) , Tousif Bhojani, ameibua shangwe kwa wakazi wa eneo hilo baada ya kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali zilizo kuwa zikiwakabili.
Bhojani ametatua karo mbalimbali za wananchi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero uliofanyika katika Viwanja vya Soko la Kisutu, ambao ulihusisha pia wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali ambao walizitolea majibu baadhi ya changamoto.
Kero hizo ni pamoja na ukosefu wa kisima cha maji katika Soko la Baba na Mamalishe Kisutu, kuvuja kwa paa la soko hilo na ukosefu wa vifaa vya zimamoto.
Changamoto zingine ni maegesho, kero ya kamata kamata ya 'wrong parking', ulinzi na usalama, mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na utirikaji wa maji taka.
Katika kutatua changamoto ya Soko la Mama na Baba Lishe Kisutu kutokuwa na kisima, Diwani Bhojani aliwasiliana kwa simu papo hapo na Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Hassan Zungu, ambaye aliwahutubia wananchi kwa njia ya simu na kuahidi kushirikiana na diwani huyo kutatua kero hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu Spika Zungu amewataka wananchi kushikamana, kuwa wamoja na kuahidi kero mbalimbali kuwa zitatuliwa kwa kushirikiana na diwani wao huyo, jambo lililozua shangwe.
"Baada ya kukata simu Spika na Mbunge wetu Zungu, amenitumia ujumbe kuwa tutahakikisha kisima cha maji kina jengwa hapa.Kuhusu paa la soko kuvuja nimewasiliana hapa hapa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, ameahidi kuja mwenyewe kukagua na kuna kushughulikia kero hiyo,"amesema Diwani Bhojani.
Diwani huyo pia ameahidi kutoa kifaa cha kuzimia moto katika soko hilo mapema wiki ijayo.
Kuhusu changamoto ya ubovu wa barabara kutokana mvua iliyonyesha, Diwani Bhojani ameahidi kuiwasilisha kwa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) ili kurekebishwa.
Akizungumzia ulinzi na usalama, diwani huyo amesema kuna vikundoi vya sungusungu v kwa kushirikiana na Jeshi la polisi, vinaimarisha ulinzi katika kata hiyo hivyo kuwatoa hofu na kuwataka kuchangia ada ya ulinzi.
Changamoto zingine zilijibiwa na taasisi za serikali hususan Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, ambalo liliahidi kufanya ukaguzi katika soko hilo.
Kwa upande wa kero ya maji Mwakilishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) amewatoa wasaiwasi wananchi kuhusu upatikanaji wa maji kwamba mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha mifumo yake kuhakikisha maji yanapatikana wakati wote.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, mwakilishi kutoka jiji hilo, amesema kata hiyo imenufaika na mikopo ya jumla ya sh. milioni 169 ambazo zimetolewa kwa vikundi vitano, hivyo kuwataka wananchi kuunda vikundi kwani mikopo hiyo ipo na inaendelea kutolewa.
Wananchi wa kata hiyo wamempongeza Diwani Bhojani kwa utaratibu wa kuandaa mikutano na kusikiliza kero zao kwani ni njia rahisi ya kutatua kero hizo kabla hazijaleta adha kubwa.











Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...