Na Janeth Raphael -MichuziTv Singida
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria dhidi ya watumishi wote wa umma watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za Serikali, akisisitiza kuwa tabia ya kuwahamisha badala ya kuwakamata imekuwa ikichangia kuendelea kwa vitendo vya wizi katika maeneo mbalimbali nchini.
Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Mei 31, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Itigi mkoani Singida, ambapo ameeleza kuwa Serikali haitavumilia watumishi wanaotumia nafasi zao vibaya kwa kuiba mali na fedha za umma zilizotokana na kodi za wananchi.
Amesema watumishi wanaobainika kufanya ubadhirifu hawapaswi kuhamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine kwani hatua hiyo haina tija, badala yake huwapa nafasi ya kuendelea kufanya vitendo hivyo katika maeneo mapya wanayopelekwa.
“Mwizi wala msimuhamishe. Mkishamhamisha anaenda kuiba na huko. Wale ambao walishahamishwa, kule walikopelekwa RPC wa huko awakamate,” alisema Waziri Mkuu huku akipigiwa makofi na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Katika hotuba yake, Dkt. Mwigulu alionesha kusikitishwa na baadhi ya watumishi wa umma wanaoshindwa kutambua dhamana waliyopewa na wananchi, akibainisha kuwa wengi wao wamepata elimu kwa gharama za Serikali kupitia kodi za Watanzania na baadaye kupewa nafasi za kazi ili kulitumikia taifa.
Amesema ni jambo la kushangaza kuona baadhi yao wakitumia nafasi hizo kwa manufaa binafsi badala ya kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na uzalendo.
“Kuna watu hawamwogopi hata Mungu. Umesoma kwa kodi za Watanzania, umepata nafasi ya kuwatumikia wenzako, lakini unaamua kuwaibia. Wakati huo huo kuna vijana wengi wenye sifa wanaosubiri nafasi za ajira,” alisema.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inaendelea kupambana na vitendo vya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote.
Aidha, alihoji mantiki ya kuendelea kuwahamisha watumishi wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu huku Serikali ikibeba gharama za uhamisho wao, ikiwemo posho na nauli, jambo alilosema halina tija katika mapambano dhidi ya wizi wa mali za umma.
“Baada ya kuiba unataka tukuhamishe na tukulipie nauli ya kuhama. Hata hizo sheria tutazirejea. Mimi sichukii watu, lakini nachukia wizi,” alisisitiza.
Kauli ya Waziri Mkuu imekuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza uwajibikaji, uwazi na nidhamu katika utumishi wa umma, huku ikitaka fedha za wananchi zilindwe na kutumika ipasavyo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma za kijamii nchini.
Wakazi wa Itigi waliohudhuria mkutano huo walimpongeza Waziri Mkuu kwa msimamo wake dhidi ya ubadhirifu, wakieleza kuwa hatua kali dhidi ya wahusika zitasaidia kuongeza uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...