Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) na Wakala wa Elimu Nje ya Nchi Global Education Link (GEL) wamesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayolenga kuwatafutia wanafunzi wa chuo hicho fursa mbalimbali za kitaaluma.

Makubaliano hayo yalisainiwa jana jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa GEL, Abdulmalik Mollel, na Kaimu Mkuu wa DUCE, Profesa Pendo Malangwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi aliyemwakilisha Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Kituye, aliipongeza GEL na DUCE kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kusaidia maendeleo ya elimu na kuwaandaa vijana kwa maisha ya kazi baada ya masomo.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza sana DUCE pamoja na Global Education Link kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kusaidia maendeleo ya elimu na maandalizi ya vijana wetu kwa maisha ya kazi baada ya hatua mbalimbali za masomo,” alisema Kituye.

Aidha, alisema Dar es Salaam ni mkoa wenye nafasi kubwa katika maendeleo ya taifa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu, shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi, vyuo vya elimu ya juu, hospitali za rufaa na binafsi pamoja na viwanda vikubwa na vya kati vinavyoendelea kukua kila siku.

Alisema ukuaji huo wa uchumi na miundombinu unaongeza wajibu kwa wadau wa elimu kuhakikisha vijana wanapata maarifa, ujuzi, maadili na uwezo wa kutumia fursa zinazozidi kuongezeka ndani ya mkoa huo na taifa kwa ujumla.

“Ndiyo maana suala la kunasihi vijana kuhusu ulimwengu wa kazi baada ya masomo lina umuhimu mkubwa sana katika kipindi hiki. Kimsingi, mwanafunzi wa leo anatakiwa kujitambua mapema, kuelewa uwezo wake, mahitaji yake, ndoto zake na fursa za kazi zilizopo mbele yake,” alisema.

Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kusoma wakiwa wanajua wanachosoma, sababu za kusoma taaluma hizo na namna watakavyotumia maarifa na ujuzi wanaoupata katika maisha yao ya baadaye.

Kituye alisema bila mwongozo sahihi wa taaluma, vijana wengi huchagua masomo bila kuzingatia uwezo wao, ndoto zao na mahitaji ya soko la ajira au fursa zinazotarajiwa kujitokeza miaka ijayo.

“Kwa kuzingatia hilo, ni jambo la faraja kuona kuwa DUCE pamoja na Global Education Link wameamua kuunganisha nguvu katika eneo hili muhimu,” alisema.

“Kwa niaba ya Ofisi ya Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, napenda kuupongeza tena uongozi wa DUCE pamoja na Global Education Link kwa kuanzisha ushirikiano huu muhimu. Ni imani yangu kuwa hatua hii ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika namna tunavyowaandaa vijana wetu kwa elimu, ajira, ubunifu na maisha ya baadaye,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, alisema GEL imefikisha miaka 19 katika kazi ya kuwapa wanafunzi mwongozo wa taaluma mbalimbali za kusomea.

Alisema moja ya kazi kubwa zinazofanywa na taasisi hiyo ni kuwatafutia wanafunzi wa Tanzania fursa za kusoma nje ya nchi pamoja na kusaidia kujenga ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya ndani na vya nje kwa lengo la kuleta teknolojia na maarifa mapya nchini.

Alisema nchi zilizoendelea zimefikia mafanikio hayo kutokana na uwekezaji mkubwa katika maarifa ya wananchi wake, hivyo GEL imeona umuhimu wa kusaidia kuleta maarifa hayo Tanzania.

Mollel alisema GEL tayari imesaini mikataba ya ushirikiano na vyuo vikuu mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mzumbe, Nelson Mandela, TIA na vinginevyo, huku kusaini makubaliano na DUCE ikiwa ni mwendelezo wa juhudi hizo.

“Kila chuo tunachosaini nacho makubaliano tunakuwa na malengo maalum. Leo tumesaini na DUCE kwa ajili ya kutoa mwongozo kwa wanafunzi, na hatuishii kwa wanafunzi pekee; hata wazazi wanaotaka kujiendeleza kielimu au walimu wanaotaka kuongeza elimu tunawapa mwongozo,” alisema Mollel.

Naye Kaimu Mkuu wa DUCE, Profesa Pendo Malangwa, alisema tukio hilo linaonesha dhamira ya dhati ya kuwaandaa vijana katika maisha ya taaluma na ajira za baadaye.

Alisema kupitia ushirikiano huo, wanafunzi wa DUCE watapata mwongozo wa kitaaluma na kufahamu fursa zilizopo ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha kukabiliana na ushindani mkubwa wa soko la ajira duniani.

Profesa Malangwa alisema DUCE itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kutoa elimu bora, kufanya tafiti na kuandaa wataalamu, huku GEL ikitoa uzoefu wake katika kuwaunganisha vijana na kuwapa ushauri wa maendeleo ya kitaaluma.

Alisema ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza mwongozo wa kitaaluma, ushirikishwaji wa wanafunzi, kuwajengea uwezo pamoja na kuimarisha mawasiliano kupitia vyombo vya habari ili kusaidia vijana kuelewa taaluma mbalimbali na mahitaji ya soko la ajira.

“Sote ni mashahidi hapa kwamba vijana wengi wakimaliza kidato cha sita hawana uwezo wa kuchagua wanachotaka kusoma. Wengine wanachagua tu kwa sababu wamesikia kutoka kwa watu wengine. Kupitia ushirikiano huu tunataka vijana wachague taaluma wanazozielewa na zitakazowaletea tija katika maisha yao ya baadaye,” alisema Profesa Malangwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...