Na Said Mwishehe,Michuzi TV

HATIMAYE Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imetangaza rasmi kwamba kuanzia Julai 1 mwaka huu wa 2025 nchi yetu ya Tanzania itaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Wakati utekelezaji huo ukitarajiwa kuanza tarehe hiyo ya Julai 1, tayari upo msingi imara wa kisera, kitaasisi na kiutekelezaji unaolenga kuharakisha mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiutawala kwa miongo ijayo. 

Katika kikao chake kilichofanyika Dar es Salaam hivi karibuni chini ya Mwenyekiti wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tume ya Taifa ya Mipango iliidhinisha miongozo na mifumo muhimu ya kusimamia utekelezaji wa Dira 2050 pamoja na kuelekeza kuharakishwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayokuwa nguzo kuu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Pamoja na kuidhinisha Mwongozo wa Kitaifa wa Mipango, Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo, Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo na Mkakati wa Mawasiliano wa Dira 2050, Tume imeweka msisitizo maalum katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya uwekezaji inayotarajiwa kuchochea mabadiliko ya kimuundo katika uchumi wa Tanzania.


Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG), Mradi Unganishi wa Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma, Mradi wa Kabanga Nickel pamoja na Kiwanda cha Usafishaji Kahama, na Mradi wa Magadi Soda wa Engaruka. 

Kwa pamoja, miradi hiyo inawakilisha uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 120, sawa na takribani dola za Marekani bilioni 47.

Miradi hiyo imeainishwa kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira 2050 kwa sababu ina uwezo wa kuvutia uwekezaji mkubwa wa ndani na nje, kuongeza ajira, kuimarisha mapato ya Serikali, kukuza mauzo ya nje, kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kikanda na kimataifa.

Mradi wa LNG unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya nishati na mapato ya fedha za kigeni. 

Liganga na Mchuchuma vinatarajiwa kuweka msingi wa maendeleo ya viwanda kwa kuongeza uzalishaji wa chuma na nishati nchini. Kabanga Nickel inaipa Tanzania nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kijani unaochochewa na ongezeko la mahitaji ya madini muhimu kwa utengenezaji wa betri na teknolojia za nishati safi duniani. 


Nayo Engaruka inafungua fursa mpya katika sekta ya kemikali na viwanda vinavyotegemea malighafi za ndani.

Kwa kuzingatia malengo ya Dira 2050 ya kufikia uchumi wa takribani dola trilioni moja, miradi hiyo siyo uwekezaji wa kawaida bali ni injini za mageuzi ya kiuchumi. 

Hivyo uamuzi wa Tume ya Taifa ya Mipango wa kuipa kipaumbele utekelezaji wake unaashiria dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Dira 2050 inatafsiriwa katika matokeo halisi yatakayoongeza tija, ajira, ustawi wa wananchi na ushindani wa Taifa katika miaka ijayo.

Pamoja na hayo ukweli ni kwamba kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaonesha dhamira,kiu na shauku ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuona nchi yetu inapiga hatua zaidi katika kuleta maendeleo, kuboresha hali za maisha ya wananchi na kubwa zaidi kuifanya Tanzania kuwa injini ya kukuza uchumi wake kupitia rasilimali zake .

Unapoiangalia Dira ya Taifa ya Maendeleo unaiona Tanzania tuitakayo na safari ya kuelekea huko inaanza sasa. Hongera Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua hii inayowasha taa ya kijani yenye matumaini makubwa kwa Watanzania.

Lakini kwa muda mrefu Watanzania tumekuwa tukiitamani Tanzania itakayokuwa na uwezo mkubwa wa kuajiri watu wake kupitia sekta mbalimbali na katika Dira hiyo imeeleza kwa kina namna ambavyo nchi inavyokwenda kuimarisha sekta hizo kama mkakati wa kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania.

Kwa mfano Tume ya Taifa ya Mipango chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kikao chake cha Mei 26 pamoja na mambo mengine pia imeidhinisha sekta za kipaumbele 12 wakati wa utekelezaji wa dira hiyo.

Sekta hizo ni ya kilimo idadi ya viashiria vya upimaji katika mabano ni (15), viwanda na ujenzi (10), Madini na Nishati(10), Utalii(5), michezo na Sanaa(9), sekta ya ubunifu na maudhui ya kidigitali(2) wakati sekta ya miliki ,aridhi na maendeleo ya miji(13)

Pia sekta nyingine ni biashara na uwekezaji(12), Elimu(54), hifadhi za jamii,kazi na ustawi wa jamii(34), uchumi wa bluu(18) pamoja na sekta ya Sayansi,teknolojia,ubunifu na uchumi wa digitali(24).

Unapoangalia sekta hizo ambazo zimepewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utabaini mkakati uliopo kama nchi ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kufungua fursa zaidi ambazo kila mmoja atashiriki katika shughuli za kiuchumi na hatimaye kwa pamoja kubadilisha maisha yetu kutoka tuliyonayo sasa na kuwa na maisha bora zaidi.

Na kwa kuwa dira hiyo imelenga kubadilisha maisha yetu ni matumaini yangu wananchi wote na wa rika na kada zote tunaowajibu wa kuungana na Rais Dk.Samia na Serikali anayoiongoza katika kuwa sehemu ya safari ya kutekeleza dira hiyo ambayo ikifanikiwa kizazi kilichopo sasa na kijacho kitakuwa kwenye ile nchi ya ahadi ya asali na maziwa.

Kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaonesha jinsi ambavyo inakwenda kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na lengo ni kuwezesha pamoja na kuwa na ukuaji wa uchumi kwa ujumla kama Taifa lakini pia uchumi wa kila mmoja wetu nao ukue.Ndio mpango uliopo.

Binafsi sina shaka na Rais Dk.Samia katika kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwani kwa dhamira yake na utashi wake ndio aliyetoa maelekezo ya kuandikwa kwa Dira hiyo kazi ambayo ilifanyika kwa weledi mkubwa na kupita katika hatua mbalimbali na hatimaye sasa utekelezaji wake unakwenda kuanza rasmi.

Hata hivyo nitoe rai kwa Vyama vya siasa nao wanapaswa kuwa sehemu ya kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dira hiyo.Ni matumaini yangu kama ilivyo kwa CCM Ilani yake imeakisi kwa kiasi kikubwa yaliyomo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hivyo kwa vyama vya siasa vya upinzani kuakisi yaliyomo katika Dira hiyo kupitia Ilani zao.Lakini kwa kuwa utekelezaji wa dira unaanza Julai 1,2026 ni vema wanasiasa wetu bila kujali itikadi ya vyama wakaungana na Watanzania wote kuitekeleza dira hiyo.


Simu 0713833822


Mwisho



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...