Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia masuala ya Utawala, Katiba na Sheria imeeleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji ndani ya Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo – BEMC. Kauli hiyo imetolewa baada ya kamati kufanya ziara ya ukaguzi ili kujionea maendeleo ya shughuli mbalimbali zinazosimamiwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania, TISEZA.

Eneo la BEMC lilianzishwa kisheria kupitia Tangazo la Serikali Na. 123 la tarehe 24 Mei 2013. Lina jumla ya hekta 9,800, ambapo hekta 887 zimetengwa mahsusi kwa ajili ya Bandari ya kisasa ya Mbegani. Sehemu iliyobaki, yenye hekta 8,903, inatumiwa kwa shughuli za uwekezaji. Mradi huu unatajwa kuwa wa kimkakati kitaifa na unalenga kukuza sekta ya viwanda, biashara na uchumi kwa ujumla.

Katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa, BEMC umetambuliwa kama moja ya nguzo zitakazosaidia Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja ifikapo 2050. Kufikia Mei 2026, wawekezaji 24 tayari walikuwa wameshapatiwa maeneo na kuanza utekelezaji wa miradi yao. Miradi hiyo ipo katika hatua tofauti kama ujenzi wa viwanda, mabanda ya uzalishaji, uzio pamoja na miundombinu wezeshi.

Wakati wa ziara hiyo, Kamati ilisema imefurahishwa na kasi ya ujenzi na uwekezaji unaoendelea. Miongoni mwa miradi iliyotajwa kuvutia ni kiwanda cha Sinovest Industry Investment Limited kitakachozalisha nguo na bidhaa za nguo. Kiwanda hicho kimejengwa kwenye eneo la mita za mraba 210,080, sawa na hekta 21. Mpaka Mei 2026, uwekezaji uliofanyika ulifikia dola milioni 7 za Marekani, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 21. Kinatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mwishoni mwa Juni 2026.

Kukamilika kwa kiwanda hicho kutaleta ajira nyingi. Awamu ya kwanza itazalisha ajira 1,000 za moja kwa moja, na awamu ya pili itaongeza ajira 500. Kiwanda kitatumia mashine za kisasa kuzalisha nguo zenye ubora wa kimataifa kwa ajili ya masoko ya Marekani na Ulaya.

Uwekezaji wa aina hiyo unachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa, unaongeza thamani ya bidhaa za viwandani, pamoja na kuboresha kipato cha wananchi wa Bagamoyo, Mkoa wa Pwani na Tanzania nzima.

TISEZA inalenga kuhakikisha maeneo yote maalum ya uwekezaji yanatumika kikamilifu ili kuvutia mitaji na kuleta tija kwa wananchi. Lengo ni kuwafanya Watanzania wanufaike na fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali. Uwekezaji unabaki kuwa chombo muhimu cha kutoa ajira, kuvutia mitaji kutoka nje, kuhamisha teknolojia na kuimarisha msingi wa viwanda nchini.

Maendeleo yanayoonekana BEMC yanaonyesha nia ya dhati ya Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kusukuma utekelezaji wa miradi mikubwa yenye maslahi mapana kwa wananchi na Taifa.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...