Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza rasmi nafasi za mafunzo ya mujibu wa sheria kwa vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka 2026, huku likiwataka wote waliopangiwa kuripoti kambini kati ya Juni 1 hadi 7 mwaka huu.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, ambapo amesema maandalizi yote ya kuwapokea vijana hao katika kambi mbalimbali nchini yamekamilika.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana uzalendo, nidhamu, uwezo wa kujitegemea pamoja na kuwapa stadi mbalimbali zitakazowasaidia katika maisha na maendeleo ya taifa.
“Lengo letu ni kuhakikisha vijana wanapata mafunzo yatakayowajenga kuwa wazalendo, wenye maadili mema na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya nchi,” alisema Brigedia Jenerali Mabena.
Ameeleza kuwa JKT itaendelea kuwa sehemu muhimu ya kuwalea vijana katika misingi ya uwajibikaji, mshikamano wa kitaifa na kuthamini amani ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena, wahitimu wote wanatakiwa kuangalia majina yao pamoja na kambi walizopangiwa kupitia tovuti rasmi ya JKT ambayo ni JKT Tanzania.
Aidha, amesema Serikali kupitia bajeti ya mwaka huu imeiwezesha JKT kupokea idadi kubwa ya vijana kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajili ya mafunzo hayo.
Pia amewataka wazazi na walezi kuwapa ushirikiano vijana hao kwa kuwahamasisha kwenda kuripoti kambini ndani ya muda uliopangwa.
“Tunawaomba wazazi na walezi kuhakikisha vijana wanaripoti kwa wakati ili waweze kupata mafunzo haya muhimu kwa mustakabali wao na taifa kwa ujumla,” alisema.
Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana wenye mahitaji maalum wanapaswa kuripoti katika Kambi ya Ruvu JKT wakiwa na vifaa na nyaraka muhimu zilizoelekezwa na jeshi hilo.
Amesisitiza kuwa vijana wote waliopangiwa wanapaswa kufuata maelekezo yaliyotolewa na kuripoti katika kambi zao ndani ya muda uliopangwa ili kuepusha usumbufu wa kiutawala.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...