Na Mwandishi Maalum, Mbinga
WAKULIMA na wafanyabiashara wa kahawa wilayani Mbinga,wameishukuru kampuni ya Hagati Company Ltd kuwajengea kiwanda cha kisasa cha kuchakata kahawa Hagati Coffee ambacho kinalenga kuimarisha soko la kahawa na kuondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili wakulima wa zao hilo kwa muda mrefu.
Kiwanda hicho kimewawezesha wakulima na baadhi wafanyabiasha kuanza kuuza kahawa iliyosindikwa kwenye masoko ya ndani na nje ya wilaya ya Mbinga hivyo kuhamasisha unywaji wa kahawa kwa watu ndani na nje ya wilaya ya Mbinga.
Wakizungumza jana kuhusu faida ya kiwanda hicho mkulima wa kahawa wa kijiji cha Kipapa Astel Hili,ameipongeza kampuni hiyo kwa kuwekezakuanzisha kiwanda hicho ambacho kitasaidia kuuza kahawa iliyosindikwa badala ya kuuza kahawa ghafi kwa njia ya mnada ambayo faida yake ni ndogo ikilinganisha na kahawa iliyosindikwa.
“Naimpongeza sana kampuni ya Hagati kutuletea kiwanda hiki cha kisasa,kiukweli kwa sasa tunafanya biashara yetu ya kahawa iliyosindikwa na tunapata wateja wengi wakubwa na wadogo wanaotoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma”alisema.
Aidha alisema,kiwanda hicho kimesaidia kutoa ajira kwa baadhi ya wananchi hasa vijana ambao awali hawakuwa na kazi ya kufanya hivyo kujikuta wakidhurura mitaani na wengine kujiingiza kwenye vitendo vya uharifu.
Mfanyabiashara wa kahawa Anold Ndunguru alisema,kuanzishwa kwa kiwanda cha Hagati ni mwanzo mzuri ya safari ya matumaini kwa wadau wengi wa tasinia ya kahawa katika wilaya ya Mbinga ambao sasa watafaidika na zao hilo na kupunguza vitendo vya ununuzi wa kahawa ghafi kwa njia haramu ya magoma.
Mmiliki wa kiwanda hicho Abubakari Ali Abubakar alisema,mkakati wa Hagati Company Ltd kupitia bidhaa zake za Hagati Coffee ni kusogeza huduma bora na kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuhamasisha jamii kupenda kunywa kahawa yenye umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu.
Abubakari,alisema kunywa kahawa kuna faida nyingi ikiwemo kuongeza kinga dhidi ya ugonjwa wa ini,inapunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya akili na kisukari.
Alisema,Hagati Company Ltd inatambua changamoto ya kipato kwa Watanzania wengi,hivyo inachakata na kuuza bidhaa za kahawa kuanzia gramu 50,100,200 na kilo moja ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa gharama nafuu zaidi.
Alisema,Hagati Company Ltd itaendelea kuimarisha ushindani katika huduma zake za Hagati coffee ili kuhamasisha wananchi hata wa kipato cha chini kupenda kunywa kahawa na kuwapunguzia gharama katika matumizi ya kila siku.
Ametaja maduka yanayouza bidhaa za Hagati coffee kwa upande wa Mbinga ni Erick Shop karibu na benki ya NMB,Kilocha Shop,Songea dukani kwa Kaburu jirani na soko kuu la manispaa ya Songea na Dar es slaam duka lipo Kigamboni njia panda ya kwenda Kisota.
“wenyeji wa mkoa wa Ruvuma wanalima sana kahawa lakini suala la unywaji ni changamoto kubwa,wanywaji wakubwa wa kahawa hawapo hapa Mbinga wapo nje ya nchi na ndiyo wanaojua thamani ya kahawa hii”alisema.
Alisema,yeye ni mzaliwa wa Mbinga hivyo ameona jina sahihi la kuipandisha hadhi kahawa inayolimwa Mbinga ni jina la Hagati coffee ambalo ni bonde maarufu kwa uzalishaji wa kahawa safi inayosifika ulimwenguni kote.
Amewaomba wakulima kupitia vyama vyao vya msingi vya ushirika(Amcos)wafanyabiashara na wadau wa tasinia ya kahawa kutumikia kiwanda cha Hagati coffee kwa usindikaji ili waweze kupata kahawa bora itakayokubali kwenye soko la ndani na nje ya nchi.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...