Bagamoyo, Pwani

HISTORIA ya ustaarabu wa pwani ya Afrika Mashariki imeendelea kuvutia wageni na watalii wa ndani baada ya ujumbe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya kutembelea Magofu ya Kaole yaliyopo Bagamoyo mkoani Pwani na kueleza kuvutiwa na urithi mkubwa wa kihistoria uliopo eneo hilo.

Ujumbe huo umetembelea eneo hilo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utalii wa ndani na kujifunza historia ya taifa, huku viongozi wake wakieleza kuwa Magofu ya Kaole ni miongoni mwa maeneo yanayoonesha mchango mkubwa wa Tanzania katika historia ya biashara, dini na ustaarabu wa Afrika Mashariki tangu karne ya 13.

Katika ziara hiyo, wageni hao walipata fursa ya kutembelea misikiti ya kale inayosadikiwa kuwa miongoni mwa misikiti ya mwanzo kabisa Afrika Mashariki, makaburi ya kihistoria ya Shirazi yaliyojengwa kwa mawe ya matumbawe, kisima cha kale pamoja na mabaki ya mji wa zamani wa biashara uliokuwa ukiunganisha Afrika, Uarabuni na Asia kupitia Bahari ya Hindi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Dk. Libamba Shobo alisema Kaole ni eneo lenye thamani kubwa ya kihistoria na kitamaduni ambalo linaweza kuwa chachu ya kukuza utalii wa ndani na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu historia ya taifa.

Alisema vivutio vilivyopo katika eneo hilo vinaakisi namna Tanzania ilivyokuwa kitovu muhimu cha biashara na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali kwa karne nyingi, hali inayopaswa kutumiwa kuhamasisha kizazi cha sasa kuthamini urithi wa nchi.

“Kaole si eneo la kawaida; ni sehemu inayobeba historia ya taifa letu na ustaarabu wa mwambao wa Afrika Mashariki. Watanzania wengi wanapaswa kufika hapa kujifunza na kutambua mchango wa maeneo haya katika historia yetu,” alisema.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuhifadhi maeneo ya kihistoria na kuyaendeleza ili yaweze kuchangia zaidi katika uchumi kupitia sekta ya utalii, sambamba na kutoa elimu kwa jamii kuhusu urithi wa Tanzania.

Kwa miaka ya karibuni, Magofu ya Kaole yameendelea kuvutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na historia yake ya kipekee inayohusisha ustaarabu wa Waswahili, biashara za kale za Bahari ya Hindi pamoja na kuenea kwa dini ya Kiislamu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Bagamoyo, ambayo kihistoria ilitumika kama lango muhimu la biashara na utamaduni wa pwani, inaendelea kujijengea sifa kama moja ya maeneo muhimu ya utalii wa kihistoria nchini.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...