Na Janeth Raphael -MichuziTv Bungeni,Dodoma
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeeleza kuwa vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2026/2027 vitaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa, kikanda na kimataifa inayolenga kuimarisha maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimataifa.
Akizungumza Bungeni, leo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amesema wizara hiyo itaongozwa na nyaraka mbalimbali za kimkakati zikiwemo Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001, toleo la mwaka 2024, pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo pia utazingatia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/2027 – 2030/2031), ambao unalenga kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi kupitia sekta mbalimbali za maendeleo.
Kwa mujibu wa Waziri Kombo, mipango hiyo pia itaendana na Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (2021–2026) pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambayo imeweka malengo ya kimkakati ya maendeleo ya taifa katika kipindi kijacho.
Katika hatua nyingine, Wizara hiyo itaendelea kuzingatia mikataba ya kikanda na kimataifa ikiwemo Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 1999, Mkataba wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa mwaka 1992, pamoja na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu 2030.
Vilevile, utekelezaji wa vipaumbele hivyo utaongozwa na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063, Dira ya SADC ya mwaka 2050 na Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2050, sambamba na mikataba mingine ya kikanda na kimataifa inayolenga kuimarisha ushirikiano wa mataifa.
Waziri Kombo amebainisha kuwa Wizara pia itaendelea kuzingatia maelekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa pamoja na ushauri unaotolewa na Bunge katika kuhakikisha sera na mikakati ya diplomasia ya nchi inatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa mujibu wake, vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 vitajikita katika maeneo makuu manne, ambayo ni kuimarisha uratibu na ushirikiano wa nchi mbili, kikanda na kimataifa, pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (toleo la 2024), hususan katika eneo la diplomasia ya uchumi.
Maeneo mengine ni kulinda taswira, heshima na maslahi ya Taifa katika nyanja za kimataifa, pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Wizara, kuimarisha utawala bora, rasilimali watu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Wizara na taasisi zake.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha nafasi ya Tanzania katika majukwaa ya kimataifa sambamba na kukuza ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa manufaa ya wananchi.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...