Waziri Mkuu Mstaafu, Kassimu Majaliwa (katikati) akipiga makofi baada ya kuzindua mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Benki ya Biashara ya Mwalimu ikilenga kuongeza mtaji wa benki, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 6, 2026 Jijini Dar es Salaam
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Kassimu Majaliwa amezindua mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Mwalimu Commercial Bank (MCB), ukilenga kuongeza mtaji, uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo.
Akizungumza Dar es Salaam leo Mei 5, 2026 wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Majaliwa amesema uzinduzi wa hisa stahiki unatoa fursa kwa wanahisa wote, akiwemo yeye mwenyewe, kuongeza umiliki katika benki hiyo.
Ameeleza kupitia mpango huo, benki hiyo itaongeza mtaji wake ili kupanua huduma kwa wananchi wengi zaidi, kuimarisha utoaji wa mikopo na kuendeleza teknolojia za kidigitali na kuongeza ushirikishwaji wa kifedha nchini.
Amesema hisa stahiki itaongeza thamani ya uwekezaji wao kama wanahisa na kwamba si fursa ya kifedha pekee, bali fursa ya kuchangia ukuaji wa benki hiyo na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
"Nitoe mwito kwa wanahisa wote wa MCB tusikae pembeni. Huu ni wakati wetu wa kuonyesha imani yetu kwa benki yetu na tuchukue hatua ya kununua hisa hizi stahiki, si kwa sababu ya faida pekee, bali kwa sababu tunatambua tunajenga urithi wa kifedha kwa vizazi vijavyo," amefafanua.
Aidha, Majaliwa ameipongeza bodi na uongozi kwa busara na dira thabiti inayoweka benki hiyo katika njia sahihi ya ukuaji na kuwataka kuendelea na kasi hii ya ubunifu, uwazi na utumishi bora kwa wateja.
Naye, Mwenyekiti wa bodi ya MCB, Francis Ramadhani amesema katika zoezi la Hisa Stahiki, wanahisa wote ambao majina yao yapo kwenye rejesta ya wanahisa kufikia Mei 5, 2026, wana haki ya kununua hisa mpya tatu kwa kila hisa moja waliyonayo.
Amefafanua hisa hizo zitauzwa kwa bei ya punguzo ya Sh 110 na dirisha la ununuzi wa hisa stahiki limefunguliwa na wanahisa wataweza kununua hisa za benki kidigitali kupitia Soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) Hisa Kiganjani, Ofisi za Chama cha Walimu (CWT) na matawi na ofisi za benki ya Mwalimu.
"Hisa Stahiki ni fursa ya kipekee kwa wanahisa wa benki kununua hisa za ziada kwa bei ya punguzo kabla zoezi kufungwa. Hatua hii ni muhimu sana kwani inalenga kuimarisha mtaji wa benki, kuwezesha ukuaji endelevu wa biashara na kuboresha huduma tunazotoa kwa wateja wetu kote nchini," amesema
Amesisitiza mpango huo umepata idhini kutoka Benki Kuu (BOT) na litafanyika kwa uwazi chini ya usimamizi CMSA, DSE kwa ushirikiano na iTrust Finance Limited ambao ni washauri wao.
"Tunawahimiza wanahisa kushiriki, ili kuhakikisha kuwa benki yetu inapata mtaji wa ziada utakaosaidia kutanua wigo wa mikopo, kuimarisha huduma za kidijitali na kutimiza viwango vya kisheria vya mtaji vilivyowekwa na BOT," amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, Richard Makungwa amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, benki hiyo imefanikiwa kuongeza mali kutoka chini ya Sh bilioni 30 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 98 mwaka jana, ukuaji unaoakisi ufanisi wa usimamizi wa rasilimali na kuongezeka kwa shughuli za kibenki.
Pia amana za wateja zimeongezeka kutoka wastani wa Sh bilioni 16 hadi zaidi ya Sh bilioni 75 (2025), ikionesha imani kubwa ya wateja na wanahisa kwa benki.
"Mikopo imeongezeka kutoka Sh bilioni 16 (2019) hadi Sh bilioni 66 (2025), tukilenga wateja binafsi hususani walimu, watumishi wengine, wafanya biashara wadogo na kati (SME) ambao ni nguzo za uchumi wa Taifa," amesema.
Kadhalika, faida kabla ya kodi imeongezeka kutoka hasara ya Sh bilioni 4.8 (2019) hadi faida ya Sh milioni 487 (2025), ikiashiria mwenendo chanya wa kibiashara na usimamizi bora wa gharama.
Madhumuni ya benki hiyo ni kuongoza katika ubunifu wa huduma za kifedha, kuongeza thamani, uadilifu na uwajibikaji kwa kijamii.
"Tunajipanga kuona ukuaji endelevu wa faida kwa wanahisa wetu, kuimarika kwa huduma za kidigitali ili kuongeza ujumuishi wa kifedha na kuendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa kupitia uwezeshaji wa elimu, vijana na sekta ya uzalishaji," amesisitiza.
Waziri Mkuu Mstaafu, Kassimu Majaliwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Benki ya Biashara ya Mwalimu ikilenga kuongeza mtaji wa benki, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 6, 2026 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya MCB, Francis Ramadhani akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa uuzaji wa hisa stahiki wa Benki ya Biashara ya Mwalimu ikilenga kuongeza mtaji wa benki, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu na wafanyabiashara wadogo. Hafla hiyo imefanyika leo Mei 6, 2026 Jijini Dar es Salaam.


.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...