Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Dkt. Neema Majule, amesema Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027 inapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika utafiti wa miamba na vyanzo vya maji ili kubaini maeneo yenye maji ya kutosha, kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Dkt. Majule ameyasema hayo Mei 6, 2026 bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji, ambapo alieleza kuwa pamoja na jitihada za serikali za kutoa maji kutoka kwenye mito na maziwa, ni muhimu kufanya tathmini ya mazingira ili kuhakikisha hatua hizo haziathiri viumbe hai na mfumo wa ikolojia.
Aidha, ameshauri serikali kuboresha na kukarabati miundombinu ya maji iliyochakaa ili kupunguza upotevu wa maji na kusaidia kufikia viwango vya kimataifa, Pia ameomba Wizara kutenga mfuko maalum wa matengenezo (Maintenance Fund) utakaowezesha ukarabati wa miundombinu kufanyika sambamba na udhibiti wa upotevu wa maji.
Katika mchango wake, Dkt. Majule amesema ndoto ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma bado ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya mkoa huo, amesema wananchi wa Dodoma wana matarajio makubwa kuona mpango huo unatekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi kwa vitendo na si kubaki kwenye mipango ya maandishi pekee yaani makaratasi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...