Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amewapongeza walimu wa Mkoa wa Dodoma kwa jitihada zao zilizochangia kuongezeka kwa ufaulu katika ngazi zote za elimu kuanzia msingi hadi sekondari.
Akizungumza jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wa elimu uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Mei 6, 2026, Prof. Shemdoe amesema takwimu zinaonyesha mafanikio makubwa ya ufaulu kwa mwaka 2025 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Ameeleza kuwa ufaulu wa darasa la nne uliongezeka kutoka asilimia 94.6 mwaka 2024 hadi asilimia 95.9 mwaka 2025, huku darasa la saba ukipanda kutoka asilimia 87.8 hadi asilimia 93.2. Kwa upande wa kidato cha pili, ufaulu uliongezeka kutoka asilimia 86.12 hadi 88.9, kidato cha nne kutoka asilimia 92.8 hadi 94.4, na kidato cha sita kutoka asilimia 99.86 hadi asilimia 99.87.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wanafunzi, viongozi na wadau wa elimu, akibainisha kuwa kaulimbiu ya mkoa huo kwenye sekta ya elimu isemayo “Uwajibikaji wangu ni msingi wa kuinua ubora wa elimu Dodoma” imechangia kwa kiasi kikubwa kutoa hamasa.
Prof. Shemdoe amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwajibikaji katika sekta ya elimu kwa kusimamia taaluma, kudhibiti utoro wa walimu na wanafunzi, pamoja na kuhakikisha miradi ya ujenzi wa madarasa, shule mpya na vyoo inakamilika kwa wakati.
Aidha, amewataka viongozi kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya elimu zinatumika kama zilivyokusudiwa, huku akihimiza ubunifu na bidii kazini ili kuongeza mafanikio zaidi.
Aidha Waziri Shemdoe amepinga vikali swala la ubaguzi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na kuwataka walimu kuhakikisha wanafunzi hao wanapata haki sawa ya elimu, pia amesisitiza umuhimu wa huduma ya chakula mashuleni, akiwataka wazazi kushiriki katika kuchangia chakula na Walimu kutumia maeneo ya shule kwa kilimo kwaajili yao na mengine kwaajili ya Wanafunzi ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha uhakika.
Katika suala la nidhamu, Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa adhabu kwa wanafunzi zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia umri na kosa alilofanya mwanafunzi, sambamba na kufuata miongozo iliyopo badala ya maamuzi binafsi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema mkoa huo umeendelea kunufaika na maboresho ya sekta ya elimu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na kuboreshwa kwa maslahi ya walimu.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha Dodoma kupanda kutoka nafasi ya kumi hadi nafasi ya pili kitaifa kwa ufaulu, huku lengo likiwa kushika nafasi ya kwanza.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Khatibu Kazungu, ameeleza kuwa mkutano huo umelenga kutathmini utekelezaji wa mpango mkakati wa elimu wa mwaka 2025, akibainisha kuwa utoaji wa tuzo kwa walimu umeendelea kuwa chachu ya kuongeza ari ya kazi na kuboresha matokeo ya wanafunzi kila mwaka.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...