Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni - Dodoma

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava, ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuharakisha uimarishaji na usambazaji wa mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa ardhi nchini ili kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Akizungumza bungeni leo wakati akichangia mjadala wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/27, Mnzava amesema kuwa licha ya Serikali kuanza hatua za matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa ardhi, bado halmashauri chache pekee ndizo zimefanikiwa kufikiwa na mfumo huo, jambo linalochangia kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema mfumo huo unapaswa kusambazwa katika halmashauri zote nchini ili kurahisisha usimamizi wa taarifa za ardhi, kuongeza uwazi katika umiliki wa maeneo na kusaidia wananchi kupata huduma kwa haraka zaidi.

“Mpaka sasa ni halmashauri chache sana ambazo zimefanikiwa kupata mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa ardhi. Serikali inapaswa kuhakikisha mfumo huu unasambazwa nchi nzima ili kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza ufanisi katika sekta hii muhimu,” amwsema Mzava.

Mbunge huyo alikiri kuwa utekelezaji wa mpango huo unahitaji fedha nyingi, lakini akasisitiza kuwa umuhimu wa sekta ya ardhi kwa uchumi wa taifa unapaswa kupewa kipaumbele maalum.

Amesema mapato yanayotokana na kodi na pango la ardhi yanaweza kutumika kusaidia kuendeleza mifumo hiyo ya kisasa, huku akiishauri Serikali kuhakikisha sehemu ya fedha zinazokusanywa na Wizara ya Ardhi zinabaki wizara hiyo ili kusaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi na kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato zaidi.

“Kazi ya kusambaza mfumo huu nchi nzima siyo ndogo, ninafahamu kutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Lakini kutokana na umuhimu wa sekta ya ardhi, naiomba Serikali mapato yanayotokana na kodi na pango la ardhi yarudishwe kwa kiwango kikubwa zaidi wizara husika ili waweze kuendelea kutengeneza mifumo na kuboresha ukusanyaji wa mapato,” amesisitiza.

Mnzava ameeleza kuwa katika baadhi ya nchi zilizoendelea, sekta ya ardhi imekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali zinazotokana na umiliki na matumizi ya ardhi, hivyo Tanzania nayo inaweza kunufaika zaidi iwapo itawekeza vya kutosha katika mifumo ya kisasa ya usimamizi wa ardhi.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa juhudi zake za kuongeza makusanyo ya mapato na kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi, huku akiitaka Serikali kuendelea kuiwezesha wizara hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

“Tunaona kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Ardhi katika kuongeza makusanyo ya Serikali. Sasa ni wakati wa Serikali kuendelea kupeleka fedha zaidi kwa wizara hiyo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuendelea kulitumikia taifa,” alisema.

Kauli ya mbunge huyo imekuja wakati ambapo Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa ardhi na upangaji wa matumizi bora ya maeneo nchini.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...