Na Janeth Raphael- MichuziTv- Dodoma

Mbunge wa Viti Maalum, Nasria Nassir Ally, ameishauri Serikali kuandaa matamasha mbalimbali ya kimataifa yatakayosaidia kuitangaza Tanzania katika sekta ya utalii sambamba na kuongeza mapato ya taifa kupitia vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Nasria amesema kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya kipekee vinavyoweza kuvutia watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani, lakini bado kuna haja ya kuongeza nguvu katika eneo la matangazo na kampeni za kuitangaza nchi kimataifa ili kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na sekta hiyo muhimu ya uchumi.

Akichangia hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Bungeni jijini Dodoma, mbunge huyo amesema kuwa balozi wa kweli wa utalii si Serikali pekee, bali pia Watanzania wote wakiwemo watu wenye ulemavu ambao wana uwezo mkubwa wa kuitangaza Tanzania kimataifa.

“ Mimi ni balozi wa masuala ya utalii nchini, hivyo nawaomba mabalozi wetu walioko katika nchi mbalimbali duniani watuwakilishe vyema kwa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake,” amesema Nasria.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Serikali kuandaa matamasha makubwa ya utalii, sanaa na utamaduni yatakayovutia wageni kutoka ndani na nje ya nchi huku yakitumika kama jukwaa la kutangaza hifadhi za taifa, maeneo ya kihistoria, fukwe, milima pamoja na urithi wa utamaduni wa Tanzania.

Nasria amesema mataifa mengi duniani yamefanikiwa kukuza sekta ya utalii kwa kutumia matamasha, maonesho na kampeni maalum za kimataifa zinazoshirikisha watu wa kada mbalimbali katika jamii, jambo ambalo Tanzania nayo inaweza kulitumia kuongeza ushindani wake katika soko la utalii duniani.

Katika mchango wake, mbunge huyo pia aliiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha miundombinu katika maeneo ya utalii ili kuwezesha watu wenye ulemavu kupata fursa sawa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Alieleza kuwa katika baadhi ya nchi zilizoendelea, maeneo ya utalii yamewekewa miundombinu rafiki inayowasaidia watu wenye ulemavu kutembelea vivutio kwa urahisi, ikiwemo kupanda milima, kutembelea hifadhi na kushiriki shughuli mbalimbali za utalii bila changamoto kubwa.

“Tusiwachoke watu wenye ulemavu. Wapo na wana uwezo mkubwa wa kuitangaza nchi yetu kikamilifu licha ya changamoto walizonazo. Tukiwajengea mazingira rafiki watakuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya sekta ya utalii,” amesema.

Ameongeza kuwa kuboresha miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu kutasaidia pia kuvutia watalii wenye mahitaji maalum kutoka mataifa mbalimbali, hatua ambayo inaweza kuongeza mapato ya sekta ya utalii na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazojali.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...