Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, amemwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Hanifa Suleiman Hamza, kuchukua hatua kali za kuwaondoa mara moja watu wanaofanya biashara kiholela katika eneo la Daraja la Tanzanite, hususan jirani na makazi ya mabalozi jijini Dar es Salaam.
Aidha, amemwelekeza mkurugenzi huyo kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kuwaondoa ombaomba wote katika makutano ya Barabara ya Kinondoni na Ali Hassan Mwinyi, akieleza kuwa shughuli wanazofanya katika eneo hilo kwa kiasi kikubwa zinatweza utu wa binadamu.
Meya Mnyonge alitoa maelekezo hayo leo Mei 28, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
OPERESHENI OMBAOMBA
“Mkurugenzi, wimbi la ombaomba limeendelea kuongezeka Kinondoni. Baadhi ya maeneo yamekuwa kero kubwa kwa ombaomba, wengine ni watoto waliotakiwa kwenda shule, Eneo la Barabara ya Kinondoni karibu na Ubalozi wa Urusi na Benki ya Stanbic mkafanye mkakati waondolewe pale,” amesema Meya Mnyonge.
Ameeleza kuwa katika eneo hilo watu wanaojihusisha na ombaomba wamekuwa wakipika, kufua na kulala, huku baadhi yao wakiwa ni watoto wadogo.
“Watoto wanagonga vioo vya magari kuomba na wengine wanafuta vioo, hali inayohatarisha hata usalama wao. Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa afanye mkakati waondolewe.”
Kuhusu ongezeko la wafanyabiashara katika eneo la Daraja la Kisasa la Tanzanite, hasa upande wa makazi ya mabalozi, Meya Mnyonge amesema eneo hilo limegeuzwa soko kinyume cha utaratibu.
“Daraja la Tanzanite katika nyumba za mabalozi pamegeuzwa soko. Pale kuna mabalozi. Eneo hilo wameligeuza soko la kufanya biashara mpaka usiku, Watu wanaokesha pale wanajisaidia wapi? Hii ina maana wao ndiyo wanahusika na uchafuzi wa mazingira, Inatweza utu wa binadamu Lile eneo siyo soko waondolewe.”
Amebainisha kuwa ongezeko la watu wasioeleweka katika maeneo hayo linawatia hofu mabalozi, kwani huenda hata watu wenye nia ovu wakajichomeka miongoni mwa wafanyabiashara hao.
Katika hatua nyingine, Meya Songoro ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuanza operesheni ya kuondoa magari mabovu yaliyokuwa yameegeshwa katika maeneo ya watembea kwa miguu kwenye Barabara ya Tandale.
“Magari yameondolewa, sasa Tandale unaweza kupita pande zote za barabara. Tunachofanya sasa ni kuwatafutia eneo maalumu watu waliokuwa wanafanya biashara ya kuuza magari hayo mabovu, Hatuwezi kuwaondoa kwa sababu bado hatujapata eneo la kuwapeleka. Kilichofanyika ni magari hayo kuondolewa katika eneo la barabara na kusogezwa katika makazi yao.”
MARUFUKU GURIO BIAFRA
Meya Mnyonge pia amemwelekeza Mkurugenzi Hanifa kufunga shughuli zote za biashara zisizo rasmi katika eneo la viwanja vya Biafra.
“Biafra imegeuzwa gurio. Hakuna gurio pale. Unafika wakati wanafunga mpaka barabara. Kama kuna mtu ameweka gurio pale, liondolewe. Lilianza kidogo sasa limefika mpaka Msikiti wa Mtambambani.”
RASIMU YA SHERIA NDOGO YAPITISHWA
Katika hatua nyingine, Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni limepitisha Rasimu ya Sheria Ndogo za Manispaa hiyo ya mwaka 2026.
“Tumepitisha Rasimu ya Sheria Ndogo ya Manispaa ya Kinondoni inayozingatia Sura ya 288 ya mwaka 2023. Rasimu hii inahusisha vyanzo mbalimbali vya mapat”.
Amesema sheria hizo ndogo ni pamoja na Sheria ya Ada na Ushuru ya Manispaa ya Kinondoni ya mwaka 2026, ambayo pia inawataka watu wenye mabwawa ya kuogelea ya kibiashara kulipia ushuru wa shilingi 100,000 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa rasimu hiyo itaanza kutumika mara baada ya kupitishwa na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, kuwa sheria rasmi.
.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...